Na. Joseph Katonga - Arusha
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, ambaye ndiye Mgeni rasmi katika Siku ya Kimataifa ya Wanawake nchini, amesisitiza umuhimu wa mshikamano na usawa wa kijinsia katika kufanikisha maendeleo kwa kila mmoja na taifa kwa ujumla.Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyasema hayo kwa maelfu ya wananchi walioudhuria maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika leo tarehe 08 Machi 2025, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Mkoani Arusha.
Akizungumza na wananchi waliohudhuria, alisema:
"Mmedhihirisha kwamba wanawake ni jeshi kubwa na la kuaminiwa, pia niwashukuru wanaume wote waliopo hapa, wamekuwa nasi wiki nzima ya maandalizi kuelekea kilele cha siku hii ya Wanawake. Tunawashukuru sana kwa kutushika mkono."
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alieleza kuwa hatua nyingi za kisera na kisheria zimechukuliwa na zinaendelea kuboreshwa ili kuhakikisha wanawake wanapata nafasi kubwa katika jamii na kwenye maamuzi.Aidha, alirejea maazimio ya Mkutano Mkuu wa Beijing wa mwaka 1995, ambapo mataifa yaliweka malengo ya kufanikisha usawa wa kijinsia. Tanzania imefanikiwa kupiga hatua katika:
✅ Kupunguza umasikini
✅ Kupunguza na kuondoa njaa
✅ Kuboresha sekta ya afya
✅ Kuboresha elimu na nafasi ya wanawake katika jamii
✅ Kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani aligusia pia suala zima maadili na kuwaasa wananchi wote waliohudhuria sherehe kuwa ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha anakuwa na maono ya jamii iliyo bora na iliyojengeka kwa msingi imara wa kimaadili, maadili yaliyomema na yatakayochochea ushirikiano miongoni mwa watu, alihimiza kwa kusema kuwa suala la maadili sio suala la serikali pekee bali ni suala la kila mmoja wetu, taasisi binafsi, taasisi za kidini nk.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Dkt. Samia alizungumzia Umuhimu wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, akiwataka wanawake kuwa mstari wa mbele kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na kushiriki kikamilifu kwa amani na utulivu.
Maadhimisho haya ya Siku ya Wanawake Duniani 2025 yamefanyika kitaifa Mkoani Arusha, yakiwa ni chachu ya kuwapa wanawake nafasi katika sekta mbalimbali za maendeleo. Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna P. Makakala, aliongoza wanawake wa Idara ya Uhamiaji kushiriki katika maadhimisho hayo, yaliyobebwa na kauli mbiu:"Wasichana na Wanawake 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji."
#UhamiajiUsalamaNaMaendeleo🇹🇿 #MjueJiraniYako🇹🇿 #Wanawake2025 #UsawaNaUwezeshaji