Moshi, Kilimanjaro
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji cha
Kikanda (TRITA), Kilichopo Moshi Mkoani Kilimanjaro Naibu Kamishna wa Uhamiaji
(DCI) Abdallah Ramadhan Towo amewataka washiriki wa mafunzo ya usimamizi wa
masuala ya Ki-Uhamiaji kwa taasisi za Umma na Sekta Binafsi kutojihusiha na
Rushwa.
Ameyasema hayo mapema leo katika hafla
ya kufunga mafunzo hayo ya siku 05 kwa washiriki kutoka katika taasisi
mbalimbali za umma na sekta binafsi Kundi la 10 (Oparesheni Uhuru) ambapo amewataka kuwa waadilifu na kamwe wasijaribu kutoa wala kupokea Rushwa .
“Ndugu Wahitimu; mara nyingi sana Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na
Usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli amekuwa anakemea vitendo vya Rushwa, hivi karibuni alipokuwa
akiwaapisha Mawaziri na Manaibu mawaziri, alilisitiza uadilifu na pia alikemea
vitendo vya Rushwa” Alisema DCI Towo.
Kaimu Mkuu huyo wa Chuo DCI Towo aliwakumbusha wahitimu
kwamba, rushwa ni tatizo kubwa linalozorotesha ustawi wa jamii duniani kote, aidha,
kwa upande wa Afrika na nchi zinazoendelea tatizo la rushwa limeonekana kuleta
athari zaidi katika ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Hivyo ameisitiza kwamba Mafunzo waliyoyapata chuoni
TRITA yakawasaidie kuhakikisha kuwa wanaendelea kuwa wazalendo kwa kumsaidia
Mhe. Rais Magufuli katika juhudi zake za kuipandisha nchi yetu kiuchumi na
katika mikakati yake ya maendeleo pamoja na kuhakikisha kwamba miradi yote
inafanikiwa ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania.
Kwa upande mwingine, DCI Towo Kwa niaba ya Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala, ameushukuru Uongozi wa HIFADHI YA MLIMA KILIMANJARO -
KINAPA kwa kuendelea kushirikiana na Chuo kwani wamekuwa wakitoa fursa ya
mara kwa mara kupeleka washiriki katika hifadhi hiyo lakini pia mara zote
wamekuwa wakiandaa darasa maalum kwa washiriki kujifunza na hivyo, ameomba uhusiano
huo uzidi kuleta chachu ya maendeleo kwa taasisi za umma na binafsi na kwa
maslahi mapana ya taifa.
“Nampongeza sana Ndugu Paul Kayanda kwa maneno yake ya busara aliyoyatoa alipokuwa anatoa neno la shukurani kwa niaba yenu, nimefarijika sana kuona kwamba nanyi mmeona umuhimu wa mafunzo ya namna hii, msisahau kuwaeleza wengine juu ya mafunzo haya, na natumaini mtatusaidia sana kupata mawasiliano yao ili nao tuweze kuwatumia mwaliko” Alisema.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Wahitimu Bw. Paul Kayanda ammepongeza na Kumshukuru Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania Dkt. Anna Makakala kwa Kuanzisha Programu hiyo ya Mafunzo ya usimamizi wa masuala ya Ki-Uhamiaji kwa taasisi za Umma na Sekta Binafsi kwani ni msaada mkubwa sana kwao katika kurahisha utendaji wa kazi zao sanjari na kuimarisha Ulinzi na Usalama wa Taifa.
Mafunzo haya ambayo bado yanaendelea kuendeshwa kila mwezi, hivi sasa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda – TRITA kinaandaa mafunzo mengine maalum ambayo yatawakutanisha washiriki wa makundi yote kumi ambayo tayari yamepata mafunzo ya namna hii, mipango na taratibu zingine zikikamilika basi mwaliko utatumwa kwa washiriki wote.
HABARI PICHA NA MATUKIO
 |
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA), Moshi Naibu Kamishna wa Uhamiaji (DCI) Abdallah Towo akiwa katika Picha ya Pamoja Wahitimu wa mafunzo |
|
 |
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Moshi Naibu Kamishna wa Uhamiaji (DCI) Abdallah Ramadhan Towo akiongea na Vyombo vya Habari |
 |
Mkuu wa Itifaki na Uhusiano Mrakibu Leslie Mbotta akiongoza itifaki katika hafla ya kufunga Mafunzo ya Masuala ya Ki-Uhamiaji |

 |
Washiriki wakipokea vyeti |
 |
Bw. Paul Kayanda akitoa Shukrani kwa niaba ya Wahitimu |


 |
Mhifadhi Idara ya Utalii KINAPA Herman Mtei Akitoa Historia ya Mlima Kilimanjaro kwa Washiriki wa Masuala ya Ki-Uhamiaji
|
 |
Mhifadhi Idara ya Utalii KINAPA Herman Mtei Akitoa maelezo ya Mlima Kilimanjaro kwa Washiriki wa Masuala ya Ki-Uhamiaji |
 |
(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu) |