Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

12 Januari 2022

#JESHI LA UHAMIAJI LANG’ARA GWARIDE LA MIAKA 58 MAPINDUZI ZANZIBAR

 Na Inspekta Asha Ali Faki, Zanzibar

Jeshi la Uhamiaji kwa mara ya kwanza limeshiriki Gwaride la Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyoadhimishwa leo katika Uwanja wa Amani Mjini Unguja ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi alikua Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo.

Katika kuadhimisha siku hii vyombo vya ulinzi na usalama vilishiriki katika gwaride hilo la Miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar ambapo Kwa Jeshi la Uhamiaji ilikuwa ndio mara yake ya kwanza kushiriki  hatimae kuingia katika historia ya mapinduzi hayo,  vyombo vingine vya ulinzi na usalama vilivyoshiriki gwaride hilo  ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, KMKM, Mafunzo, Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), KVZ na  Jeshi la Zimamoto na Uokozi.

Gadi ya Uhamiaji iliratibiwa na Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Makame Issa Haji na kuongozwa na Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Zawadi Phanuel Chazuka akisaidiwa na Mkaguzi wa Uhamiaji David Nashon Jirabi pamoja na Mkaguzi wa Uhamiaji Getruda Joseph Melkior, Sameja wa Gadi alikuwa ni Sajini Yohana Daudi Nyumbu.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na viongozi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Majaji, viongozi wastaafu, wabunge wa Bunge la Afrika ya Mashariki, Mabalozi wa nchi mbali mbali, viongozi wa kidini, viongozi wa vyama vya siasa pamoja na Wananchi mbali mbali.

Sherehe hizo pia zilipambwa na ngoma za asili pamoja na maandamano ya wananchi wa Mikoa yote ya Unguja na Pemba, Watumishi wa afisi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, makampuni binafsi, kikundi cha Young Pioneer na chipkizi ambavyo vilinogesha sherehe hizo.

Baada ya maadhimisho hayo Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Masoud Sururu kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala ambae kutokana na itifaki alilazimika kuondoka muda mfupi baada ya kumalizika sherehe hizo, aliwapongeza viongozi, Maafisa na Askari waliocheza gwaride hilo kwa umahiri mkubwa waliouonesha.

Dkt. Makakala alifurahishwa na nidhamu, utii, uhodari, utayari na weledi wa hali ya juu wa askari hao katika kipindi chote cha mazoezi hadi kufikia kilele cha sherehe hizo sanjari na upya wake katika uwanja wa Paredi, aliwataka kuendelea na  bidii, juhudi na ari waliyoionesha katika sherehe hizo iiendelezwe katika sherehe zijazo ili kulifanya Jeshi la Uhamiaji kuwa mfano wa kuigwa katika uchezaji wa Gwaride.

 Mwisho aliwashukuru viongozi, maafisa na askari hao kwa uvumilivu waliouonesha katika kipindi chote cha maandalizi ya gwaride la Miaka 58 ya Mapinduzi na kuwakumbusha “Uaskari ni kazi ya kujitolea’’.

HABARI PICHA NA MATUKIO

  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akikagua Gadi ya Uhamiaji wakati wa sherehe ya Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar

Kikundi cha Askari wa kiume cha Jeshi la Uhamiaji kikipita mbele ya Mgeni Rasmi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati wa Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar


Kikundi cha Askari wa kike cha Jeshi la Uhamiaji kikipita mbele ya Mgeni Rasmi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati wa Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar







Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Masoud Sururu (Katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Gadi ya Uhamiaji iliyoshiriki gwaride la Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar Kulia kwake ni Kamishna wa Uhamiaji Divisheni ya Pasipoti na Uraia Gerald Kihinga na kushoto kwake waliokaa ni Kmishna wa Uhamiaji Fedha na Utawala Hamza Shabani


(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Zanzibar)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni