Na. Konstebo Amani Mbwaga, Dodoma
Waziri Mpya wa Mambo
ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Y. Masauni (Mb) na Naibu Waziri Mpya Mhe. Jumanne
A. Sagini (Mb) wamewasili leo katika Ofisi ya Makao Makuu ya Wizara iliyopo
Mtumba Jijini Dodoma na kupokelewa na watumishi wa Wizara hiyo na baadhi ya
watendaji kutoka katika taasisi mbalimbali zilizopo chini ya Wizara hiyo
ikiwemo Jeshi la Uhamiaji ambalo liliwakilishwa na Kamishna wa Uhamiaji Fedha
na Utawala Kamishna Hamza Shaban.
Akiongea na Watumishi
Wizarani hapo Mhe. Masauni alisema amefurahi kurudi kwenye familia yake kwani
miaka ya nyuma aliwahi kuwa Naibu Waziri Wizarani hapo na hivyo amewataka
watumishi hao kushirikiana ili kumsaidia Mhe. Rais katika kutekeleza adhma yake
ya kuwatumikia watanzania na kuwaletea maendeleo.
Kabla ya uteuzi huo
Mhe. Masauni alikuwa Naibu Waziri Wizara ya Fedha na Mipango.
Kwa upande wake Naibu
Waziri Mpya wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini amewashukuru
watumishi wa wizara kwa mapokezi mazuri na amewaahidi kutumia uzoefu wake wa
utumishi wa umma kwa muda miaka zaidi ya 30 kuleta mabadiliko chanya wizarani
hapo kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.
Mhe. Sagini pia ni
Mbunge wa Jimbo la Butiama lililoko Mkoani Mara.
Viongozi hao
waliwasili katika ofisi za Wizara mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan jana tarehe 10
Januari 2022 Ikulu Chamwino Jijini Dodoma.
Aidha viongozi wengine walioteuliwa kubaki katika nafasi zao katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni Katibu Mkuu Ndugu. Christopher Kadio na Naibu Katibu Mkuu Ndugu. Ramadhani Kailima.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaundwa na taasisi mbalimbali ikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA huku ikiwa na Majukumu ya Kulinda Usalama wa Raia na Mali zao , Kuhifadhi na Kurekebisha Wafungwa, Kudhibiti Uingiaji na Utokaji wa Raia na Wageni, Kutoa huduma za Zimamoto na Uokoaji, Kuwahudumia Wakimbizi, na Kuandaa Vitambulisho vya Taifa.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Waziri Mpya wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Y. Masauni (Mb) akisalimiana na Kamishna wa Uhamiaji Fedha na Utawala Hamza Shabani alipowasili katika ofisi za Wizara Mtumba Jijini Dodoma |
|
Kamishna wa Uhamiaji Fedha na Utawala Hamza Shabani |
|
Picha ya Pamoja |
Waziri Mpya wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Y. Masauni (Mb) akiwa na Mkewe baada ya kuwasili jana katika Ofisi ya Makao Makuu ya Wizara iliyopo Mtumba Jijini Dodoma. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni