Matangazo

📢 IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA — KARIBU KWENYE BLOG RASMI   ✦   📰 UHAMIAJI HABARI BLOGU — TUNAKULETEA MATUKIO KILA SIKU   ✦   📲 FUATA IDARA YETU KATIKA MITANDAO YA KIJAMII   ✦   ✉️ WASILIANA NASI: info@immigration.go.tz   ✦   ☎️ +255-22-2850575/6

31 Agosti 2019

IDARA YA UHAMIAJI YATAKIWA KUJIIMARISHA KATIKA KUVUTIA WAWEKEZAJI NCHINI








Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe Kangi Lugola ameitaka Idara ya Uhamiaji kuimarisha uwekezaji nchini. Wito huo umetolewa leo Mjini Moshi wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Uhamiaji Waandamizi  unao lenga kujadili na kutathmini utendaji kazi wa Idara ya Uhamiaji.

Akizungumza na Maafisa hao, Waziri Lugola amesisitiza kuwa nchi yetu inazo fursa nyingi za kiuchumi na Utalii hivyo kuwavutia wageni na wawekezaji wengi kuiingia na kuwekeza nchini.

“Katika utendaji kazi wake,Idara ya uhamiaji ndio kioo/taswira ya nchi yetu hivyo  tufanye kazi kwa weledi na kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kuwahudumia wageni kwa ukarimu, lugha za staha na msiwe kikwazo cha uwekezaji na utalii nchini” alisema Waziri Lugola.

Aidha, Waziri Lugola amemuagiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kusimamia kikamilifu Ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali na kudhibiti mianya inayopelekea upotevu wa maduhuli.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjro, Mhe. Anna Mghwira ametoa wito kwa Idara ya Uhamiaji kushiriki kikamilifu katika zoezi la uandikishaji na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

“Mkoa wa Kilimanjaro una idadi kubwa ya Wahamiaji haramu kutokana na jiografia yake pamoja na kuwepo kwa fursa mbalimbali za uwekezaji na utalii. Ili kukabiliana na changamoto hii, Idara iimarishe udhibiti wa mipaka ya nchi yetu ikiwa ni sambamba na kuwatambua Watanzania na raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini”, aliongeza Mhe. Mghwira.

Mhe. Mghwira ameitaka pia Idara ya Uhamiaji kujenga mahusiano na Wananchi ili kupata taarifa za haraka na sahihi kutoka kwa wananchi hao.

“Nitoe wito kwa Idara ya Uhamiaji kubuni mbinu na mikakati kwa Maafisa wake kushuka chini kwa Wananchi ili kuwa karibu zaidi na jamii na Watanzania kwa ujumla. Kwa kufanya hivyo Wananchi watajua haki zao ikiwa pamoja na kufahamu vielelezo vinavyotakiwa katika kupata huduma za Idara ikiwamo Pasipoti sanjali na kutoa taarifa juu ya uwepo wa wahamiaji haramu katika maeneo yao  amesisitiza Mhe. Mghwira.

Awali akimkaribisha Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika Mkutano huo, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala amesema kuwa Idara imezindua mpango mkakati wa kudhibiti Uhamiaji nchini. Mpango huo unalenga kuwatambua na kuwaorodhesha wahamiaji wote nchini na zoezi hilo litafanyika nchi nzima kwa kuanzia Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika utekelezaji wake, mpango huo utahusisha Viongozi wa Serikali za Mitaa au Vijiji (MEO/VEO), Maafisa Watendaji wa Kata (WEO) na kuratibiwa na Idara ya Uhamiaji. Kupitia Mpango huo Idara itaimarisha udhibiti na usimamizi wa mipaka yetu, kuimarisha ulinzi na Usalama na pia kulipatia ufumbuzi suala la Wahamiaji Walowezi. 

30 Agosti 2019

WAZIRI LUGOLA KUFUNGUA MKUTANO WA MAAFISA UHAMIAJI WAANDAMIZI


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Kangi Lugola kesho Jumamosi tarehe 31 Agosti anatarajiwa kufungua mkutano wa Maafisa Uhamiaji Waandamizi kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.  

Akitoa taarifa hiyo mjini Moshi leo, Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Mrakibu Mwandamizi Alhaji Ally Mtanda amesema kuwa mkutano huo wa siku mbili chini ya Uenyekiti wa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala utafanyika katika Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji (TRITA) mjini Moshi una lenga kujadili na kutathmini utendaji kazi wa idara pamoja na kukumbushana masuala mbalimbali hususan Sheria, Kanuni na Taratibu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na raia wa kigeni.

“Mkutano huu utahudhuriwa na Makamishna wa Uhamiaji, Maafisa Uhamiaji Mikoa yote Tanzania na Zanzibar, Wakuu wa Vitengo pamoja na Wafawidhi wa Vituo vya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Namanga, Tunduma na Bandari ya Zanzibar.” Aliongeza Alhaji Mtanda.  




14 Mei 2019

IDARA YA UHAMIAJI YAIKABIDHI SUMAJKT MRADI WA UJENZI WA JENGO LA MAKAO MAKUU DODOMA

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna P. Makakala jana alikabidhi  Mradi wa Ujenzi wa jengo la ghorofa nane ambalo litakuwa Makao Makuu mpya ya Uhamiaji  eneo la NCC, Kitalu na 18 na 19, jijini Dodoma  kwa wakandarasi wa SUMAJKT.
Kamishna Jenerali alisema " tunaijua sifa ya SUMAJKT kupitia mifano mbalimbali ya  majengo bora ambayo wameyakamilisha kwa wakati, na kwa ukweli huu nina imani kubwa nao ya kwamba jengo letu litajengwa kwa ustadi wa hali ya juu na hivyo kuwa ni moja ya majengo ya kisasa yanayovutia hapa jijini Dodoma"
 Kwa upande mwingine tukio hili lilihudhuliwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa SUMAJKT na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Martin Busungu na Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT, Kanali Mabele ambaye aliahidi kuwa shirika lake litajenga jengo ambalo litakuwa ni kioo cha ubora wa kazi zao na kwamba watu hawata hitaji kwenda jijini Dar es Salaam kuona mifano ya kazi zao bali hapa Dodoma tu.
Aidha, tukio  hili  lilishuhudiwaa na Mkuu wa Timu ya washauri waelekezi wa Mradi, Dkt. Msanifu Majenzi, Isabela Mtani kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam  ambaye alisema kuwa makabidhiano ya Mradi huo wa Ujenzi kati ya Idara ya Uhamiaji ambayo ni mmiliki na SUMAJKT ambayo ni Mkandarasi yatafuatiwa na shughuli nyingi ambazo zimepangwa kwenda kwa haraka sana na bila kuathili ubora wa kazi yenyewe na jengo linalojengwa.
Mradi wa jengo hilo ambalo litakuwa kubwa kuliko lile la Kurasini, Dar es Salaam na ambalo lilikuwa Makao Makuu ya zamani linatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 18, na kuiwezesha Idara ya Uhamiaji kuanza kutumia jengo bora lenye hadhi ya kimataifa jijini Dodoma. 
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna P. Makakala (katikati) na Afisa Mtendaji Mkuu wa SUMAJKT na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Martin Busungu (kulia) kwa pamoja wakisikiliza maelezo ya vipengele vya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Uhamiaji eneo la NCC, Kitalu na 18 na 19, jijini Dodoma toka kwa Mshauri Mwelekezi wa Mradi, Dkt. Msanifu Majenzi, Isabela Mtani wa Chuo Kikuu cha Ardhi , Dar es Salaam (kushoto ) wakati wa tukio la makabidhiano ya Mradi huo wa Ujenzi kati ya Idara ya Uhamiaji ambayo ni mmiliki na SUMAJKT ambayo ni Mkandarasi. Walioketi mbele, kulia ni Kamishna wa Uhamiaji (Utawala na Fedha), Kamishna Peter Chogero na kushota ni Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT, Kanali Mabele. 

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna P. Makakala (katikati) akisisitiza jambo kwa timu za Mshauri Mwelekezi na Wajenzi wa Mradi wa Ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Uhamiaji eneo la NCC, Kitalu na 18 na 19, jijini Dodoma. Walioketi, kulia  ni Afisa Mtendaji Mkuu wa SUMAJKT na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Martin Busungu na kushoto kwake ni Mkuu wa Timu ya washauri waelekezi wa Mradi, Dkt. Msanifu Majenzi, Isabela Mtani kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam wakati wa makabidhiano ya Mradi huo wa Ujenzi kati ya Idara ya Uhamiaji ambayo ni mmiliki na SUMAJKT ambayo ni Mkandarasi.  

09 Mei 2019

Epuka Msongamano, Wahi sasa! #ePassport


UHAMIAJI YATOA ONYO KALI KWA MAWAKALA (VISHOKA) WANAOTUMIA VIBANDA VYA WAJASIRIAMALI VILIVYOPO MKABALA NA OFISI YA UHAMIAJI MAKAO MAKUU KUWATAPELI WANANCHI.

Kaimu Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Hanelore Manyanga amekutana na wafanya biashara na wajasiriamali wanaofanya biashara katika mtaa wa Loliondo, Kurasini - Jijini Dar es salaam. Mtaa huo upo Mkabala na Ofisi za Uhamiaji Makao Makuu na kuna shughuli mbalimbali za biashara ikiwamo Mamalishe, Mawakili, Wapiga picha (Passport size) pamoja na watoa huduma za Stationaries.

Kamishna Manyanga amewataka wafanya biashara hao kuisaidia Idara ya Uhamiaji kupiga vita mawakala wa huduma za Uhamiaji (Vishoka ambao wanawatapeli wananchi wanaohitaji huduma za Uhamiaji katika maeneo hayo.

“Kumekuwepo na wimbi la Matapeli wanaojifanya kuwa Maafisa Uhamiaji wanawatapeli Wananchi kwa kuchukua pesa zao na kuwaahidi kuwasaidia kupata huduma za Uhamiaji ikiwa ni pamoja na Pasipoti, Viza, na Hati za Ukaazi kwa haraka. Kupitia kikao hiki nawaagiza kuwa mfanye biashara kwa mujibu wa matakwa ya leseni zenu kama inatokea kuna mtu ambaye siyo mhusika au anatumia vibanda vyenu kuwatapeli wananchi, tafadhali toeni taarifa Uhamiaji” alisema Kamishna Hanelore Manyanga

Aidha, Kamishna Manyanga aliongeza kuwa Idara ya Uhamiaji imedhamiria kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wale wote wanaojifanya Maafisa Uhamiaji na kuwatapeli Wananchi.
Wakitoa maoni yao katika kikao hicho baadhi ya wajasiriamali hao wametoa maoni yao na kuonesha kuchukizwa na vitendo hivyo ambavyo vinafanywa na watu ambao siyo waadilifu na kuchafua taswira nzuri ya Idara ya Uhamiaji na biashara zao kwa ujumla.

“Ni jambo jema kualikwa hapa kujadili suala hili, hata sisi tumekuwa tukichukizwa na hawa watu lakini tunashindwa kutoa taarifa kwani hatujui tumwambie nani, unakuta mtu anakuja pale mgahawani na mtu wanasaidiana kujaza fomu za Uhamiaji na baadae wanaondoka. Kupitia kikao hiki sasa tutakuwa tunatoa taarifa Uhamiaji lakini tunaomba tukitoa taarifa hizo zifanyiwe kazi na pia taarifa hizo ziwe siri” alisema Bi. Praise

Kupitia Kikao hicho wafanya biashara hao kwa pamoja wameahidi kushirikiana na Idara ya Uhamiaji na kuwafichua Mawakala/Vishoka wanaotumia Ofisi za mawakili, stationeries na migahawa kufanyia shughuli za Uhamiaji ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa yeyote atakayejihushisha na kazi za Uhamiaji katika maeneo yao ikiwa ni pamoja kufikishwa Mahakamani.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhamiaji, Uraia na Pasipoti Gerald J. Kihinga, ametoa wito kwa Wananchi kuwa hakuna Uwakala katika huduma zinazotolewa na Idara ya Uhamiaji. Hivyo mtu anayeomba Pasipoti ya Tanzania au Vibali vya Ukaazi anatakiwa awasilishe maombi yake kupitia tofuti ya Idara ya Idara ya Uhamiaji ambayo ni www.immigration.go.tz

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kamishna wa Uhamiaji, Uraia na Pasipoti Gerald J. Kihinga, Kaimu Kamishna wa Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Paul Eranga pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Uratibu, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Peter G. Mbaku.

Bi. Praise akichangia hoja katika kikao hicho.


Bw. Mulokozi ambaye ni mjasiriamali katika moja ya vibanda vilivyo mkabala na Ofisi ya Uhamiaji akieleza utayari wake katika kukabiliana na tatizo la vishoka wakati wa kikao hicho






Kaimu Kamishna wa Usimaizi na Udhibiti wa Mipaka, naibu Kamishna Paul Eranga akiongea wakati wa kikao hicho


Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Kamishna Hannelore Manyanga akiongea wakati wa kikao hicho

Baadhi wa wafanyabiasha na wajasiriamali wanaofanya shughuli zao mkabala na jengo la Uhamiaji Makao Makuu Kurasini wakiwa katika kikao cha pamoja na Idara ya Uhamiaji ili kutafuta suluhu la Vishoka wanaotumia sehemu zao za biashara kama ofisi


Kamishna wa Uraia na Pasipoti, Kamishna Gerald Kihinga akiongea wakati wa kikao hicho