Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

20 Desemba 2021

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahamaji yalivyofana Dodoma Naibu Waziri Chilo atoa neno

Na Konstebo Amani Mbwaga, Dodoma

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Khamis Hamza Chilo ameongoza maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya wahamaji ambayo hufanyika kila tarehe 18 Disemba ya kila mwaka, ambapo mwaka huu maadhimisho hayo yamefanyika Jijini Dodoma katika viwanja vya Mwl. Nyerere.

Mhe. Chilo akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alisema Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani katika kutambua umuhimu wa mchango wa haki wanazostahili wahamaji ndio maana mwaka huu maadhimisho hayo yamekwenda kwa kauli mbiu isemayo “Kutumia fursa za uhamiaji wa binadamu”

Siku ya wahamaji ilianza kuadhimishwa kwa mara ya kwanza duniani mwaka 2000 baada ya kutangazwa na mkutano mkuu wa umoja wa mataifa (UN General Asembly) tarehe 04 Disemba 2000 kupitia azimio hilo masuala yote yanayotambua umuhimu wa mchango na haki wanazostahili wahamiaji duniani yalipewa kipaumbele.

“Tunahitaji kuzitumia fursa za Ki-Uhamiaji kwa binadamu ili kuweza kufikia malengo yetu” alisema Mhe. Chilo

Aidha ametoa wito kwa Uhamiaji kuendeleza doria, misako na operesheni mbalimbali katika maeneo yote ya mipaka ya nchini.

"Nendeni mkaendeleze kwa sababu najua kazi huko inaendelea ya misako na doria ya kupambana na kuwasaka wahamiaji haramu lakini nendeni mkaendeleze jitihada hizi ili lengo na madhumuni tuishi kwa amani na usalama” alisema

Kwa upande wake mwakilishi wa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini ambae pia ni Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Masoud Sururu alisema tangu tarehe 15 Disemba 2021 Jeshi la Uhamiaji lilianza maadhimisho hayo kwa kuwa na maonesho ya huduma mbalimbali za kiuhamiaji sambamba na kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya uraia, pasipoti, visa, vibali vya ukaazi sanjari na masuala ya wahamiaji haramu.

“Tanzania kama ilivyo nchi mbalimbali duniani imeendelea kutumia fursa za wahamaji hususani wale wanaoingia nchini kwa kufuata sheria kanuni na taratibu za nchi, kundi hili ni muhimu sana katika katika maendeleo ya Taifa letu" alisema Kamishna Sururu.

Aliongeza Pamoja na kutumia fursa za uhamiaji wa kibinadamu Jeshi la Uhamiaji limeendelea kudhibiti wahamiaji wasio rasmi na ambao hawafuati sheria na taratibu za nchi wakati wa kuingia na kutoka nchini.

Lengo la udhibiti huo ni kuhakikisha nchi inakua salama wakati wote ili kuepukana na ujambazi, ugaidi, utakatishaji fedha na usafirishaji haramu wa binadamu.

Maadhimisho ya siku hiyo yalihudhuriwa na Wakuu wa Uhamiaji Wastaafu akiwemo Mkurugenzi wa Uhamiaji (Mstaafu) Kinemo Kihomano aliyeoongoza Uhamiaji kutoka mwaka 1997 hadi mwaka 2010, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji (Mstaafu) Magnus Ulungi aliyeongoza Uhamiaji toka mwaka 2010 hadi 2013 na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji (Mstaafu) Sylvester Ambokile aliyeongoza Uhamiaji toka mwaka 2013 hadi mwaka 2015.

Siku hiyo ya Kimataifa ya Wahamaji ilihitimishwa kwa mgeni rasmi Mhe. Naibu Waziri Chilo kukagua mabanda ya maonesho ya shughuli za kiuhamiaji na banda la IOM-Tanzania sanjari na kukutana na bendi ya Uhamiaji iliyotumbuiza katika siku hiyo ambapo aliipongeza sana kwa kuendelea kutoa burudani na elimu kwa umma juu ya masuala ya Kiuhamiaji.

HABARI PICHA NA MATUKIO

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Khamis Hamza Chilo (katikati) akipokea maandamano ya maafisa askari na watumishi rai wa uhamiaji katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahamaji iliyofanyika Jijini Dodoma katika uwanja wa Mwl. Nyerere tarehe 18 Disemba 2021

Wawakilishi wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama


Maandamano ya maaofisa askari na watumishi raia wa Uhamiaji wakiwa katika maandamano ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya wahamaji jijini Dodoma





Kamishna Mkuu wa Uhamiaji (Mstaafu) Sylvester Ambokile 

Kamishna Mkuu wa Uhamiaji (Mstaafu) Magnus Ulungi 

Kamishna Mkuu wa Uhamiaji (Mstaafu) Sylvester Ambokile kushoto akiteta jambo na Kamishna wa Uhamiaji anaeshughulikia Huduma za Sheria Kamishna Edmund Mrosso katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya wahamaji tarehe 18 Disemba 2021





Mkurugenzi wa Uhamiaji (Mstaafu) Kinemo Kihomano (Kulia) akisalimiana na Mkuu wa Kitengo cha Anuai za Jamii Uhamiaji Makao Makuu Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mwanahamis Kawina katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wahamaji iliyofanyika jijini Dodoma





Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Khamis Hamza Chilo (Kushoto) akiteta jambo na Kamishna wa Uhamiaji Divisheni ya Vibali vya Ukaazi Pasi na Visa  Marry Palmer ndc katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya wahamaji iliyofanyika tarehe 18 Disemba 2021, Jijini Dodoma katika viwanja vya Mwl. Nyerere.





Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Khamis Hamza Chilo (katikati) akipokea maelezo kutoka kwa Mrakibu wa Uhamiaji Azizi Kirondomara kuhusu huduma za kiuhamiaji katika banda la maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahamaji iliyofanyika Jijini Dodoma katika uwanja wa Mwl. Nyerere tarehe 18 Disemba 2021



















Brass Band ya Makutupora JKT ikiongoza maandamano ya maofisa askari na watumishi wa uhamiaji katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya wahamaji tarehe 18 Disemba 2021 Jijini Dodoma



(Picha zote na Konstebo Amani Mbwaga)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni