Matangazo

📢 IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA — KARIBU KWENYE BLOG RASMI   ✦   📰 UHAMIAJI HABARI BLOGU — TUNAKULETEA MATUKIO KILA SIKU   ✦   📲 FUATA IDARA YETU KATIKA MITANDAO YA KIJAMII   ✦   ✉️ WASILIANA NASI: info@immigration.go.tz   ✦   ☎️ +255-22-2850575/6

12 Oktoba 2019

Imarisheni doria maeneo yenu” Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala ametoa agizo hilo alipotembelea ofisi ya Uhamiaji Mkoa Katavi ambapo pamoja na kupata taarifa ya utendaji kazi wa ofisi hiyo na kusikiliza changamoto mbalimbali, aliendelea kusisitiza watumishi wa Idara ya Uhamiaji kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

“Nawataka muimarishe doria katika maeneo yenu hasa katika kipindi hiki tunapokaribia uchaguzi wa serikali za mitaa, maeneo haya yana makambi ya wakimbizi na walowezi. Hakikisheni hawajiingizi kwenye uchaguzi aidha kugombea nafasi za uongozi au kupiga kura.” Aliagiza Dkt. Makakala akiwa Namanyere.

“Mnafanya kazi nzuri sana pamoja na changamoto zilizopo, kila ofisi au kituo nInachopita maneno yangu ni yale yale nakumbusha tu kuwa kila mmoja ajitambue kuwa anatakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kujiepusha na vitendo vya rushwa pamoja na kuzingatia motto yetu ya Nidhamu, Upendo na Mshikamano miongoni mwenu, Uwajibikaji katika utendaji kazi wenu na kukataa rushwa” alisisitiza Dkt. Makakala.


Afisa Uhamiaji Mkoa Katavi, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Vicent Haule akisoma taarifa ya Utendaji kazi mkoa Katavi mbele ya Kamishna Jenerali Dkt. Makakala.


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya uhamiaji mkoa Katavi alipotembelea mwanzoni mwa wiki hii.



Maafisa Uhamiaji mkoa wa Katavi wakimsikiliza Kamishna Jenerali 





Kamishna Jenerali Dkt. Makakala akimsikiliza Afisa Uhamiaji Wilaya ya Nkasi Mrakibu Joseph Bulali wakati alipotembelea ofisi hiyo kuongea na watumishi
Add caption
Kamishna Jenrali akisalimiana na Maafisa wa Ofisi ya Uhamiaji Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa alipotembelea ofisi hiyo.


 








07 Oktoba 2019

“IMARISHENI MAPAMBANO DHIDI YA WAHAMIAJI HARAMU NCHINI”- Dkt. Makakala













Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala leo Jumatatu Oktoba 7, 2019 amewataka Maafisa Uhamiaji Mikoa yote nchini kuimarisha Mapambano dhidi ya Wahamiaji haramu.

Akizungumza na Watumishi wa Uhamiaji Mkoa wa Rukwa (mjini Sumbawanga), Dkt. Makakala amesema kuwa nchi yetu inaelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baadae Uchaguzi Mkuu. Hivyo Maafisa Uhamiaji Mikoa yote nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kwa kutoa Elimu kwa umma pamoja na kuhakikisha kuwa Wahamiaji haramu hawashiriki zoezi hilo.

Kwa ushirikiano na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Idara ya Uhamiaji inatarajia kutoa Elimu ya Uraia kwa kuanzia na Mikoa ya Kagera, Kigoma, Rukwa, Katavi na Geita. Maafisa Uhamiaji wote nchini wametakiwa kuandaa vipindi maalum vyenye lengo la kuwajengea uwezo na uzalendo wananchi hususan katika masuala ya Uraia.

“Kila Mwananchi anao wajibu wa kulinda usalama wa nchi yetu kwa kutoa taarifa za Wahamiaji haramu. Kumhifadhi au kumsaidia Mhamiaji haramu kupata kitambulisho cha mpiga kura na kushiriki zoezi la kupiga kura kwa ama kuchagua au kuchaguliwa ni kukosa uzalendo kwa nchi yetu” amesisitiza Dkt. Makakala.

“Taifa lolote Duniani liwe kubwa au dogo haliwezi kukamilika bila ya raia wake kwani raia hao ndio wenye nchi na wanaotakiwa kunufaika na haki zitolewazo na serikali kwa raia wake kwa mujibu wa katiba ya nchi ikiwa ni pamoja na haki ya kuchagua au kuchaguliwa katika nafasi za uongozi Kwa upande mwingine ni raia hao ndio wenye wajibu wa kulinda nchi yao” aliongeza Dkt. Makakala.

Awali akitoa taarifa ya Utendaji kazi katika Mkoa wa Rukwa, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Rukwa, Naibu Kamishna wa Uhamiaji Elizeus Mshongi ameeleza kuwa mkoa wa Rukwa unapokea idadi kubwa ya wahamiaji haramu, wengi wao wanatoka katika Mataifa ya Zambia, D.R Congo na Burundi.

Kwa kipindi cha cha kuanzia Januari hadi Agosti, 2019; jumla ya wahamiaji haramu 128 wamekamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali ikiwamo kushitakiwa na kuondoshwa nchini.

Naibu Kamishna Mshongi ameongeza kuwa Mkoa unaendesha zoezi la kuwatambua na kuwaorodhesha Wahamiaji walowezi. Kupitia Zoezi hilo jumla ya Walowezi 5,743 wametambuliwa na kuorodheshwa.

Aidha, Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa Wahamiaji walowezi wote wanaoishi nchini kujitokeza na kujiorodhesha, watakaoshindwa kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na kuondoshwa nchini.


“Tumejipanga kutoa huduma bora”, KAMISHNA JENERALI WA UHAMIAJI

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiongea na Watumishi katika Kituo cha Uhamiaji Tunduma mwishoni mwa wiki.

Kamishna wa Udhibiti na Usimamizi wa Mipaka, Kamishna wa Uhamiaji Samwel Mahirane akitoa taarifa ya utendaji kazi wa kituo cha Uhamiaji Tunduma kwa waheshimiwa Marais wa Tanzania na Zambia mra baada ya uzinduzi wa kituo cha huduma ya pamoja mpakani (OSBP) katika mpaka wa Tunduma.














Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala amewaagiza Watumishi wa Idara ya Uhamiaji kufanya kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa wakati wanapotoa huduma kwa Wananchi na raia wa kigeni.

Dkt. Makakala  ametoa wito huo ikiwa ni Utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoyatoa wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Kituo cha Pamoja cha Huduma Mpakani (One Stop Border Post - OSBP) cha Tunduma - Nakonde, tarehe Oktoba 5, 2019.

Awali Kamishna Jenerali alipokea taarifa ya utendaji kazi wa kituo hicho na amewataka kuimarisha doria maeneo ya mipakani na kushirikiana na watendaji kata na vijiji katika kuwabaini wahamiaji haramu wanaojipenyeza na kuishi katika maeneo yao.

Idara ya Uhamiaji kama mdau wa huduma mapakani hapo imeshiriki hafla uzinduzi wa Kituo hicho (Tunduma – Nakonde OSBP) uliofanywa kwa pamoja na Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Jamhuri ya Zambia, Mhe. Edger Lungu.  

Idara ya Uhamiaji imejipanga kutoa huduma bora na za kisasa mpakani hapo kwa kutumia mfumo wa Uhamiaji Mtandao (e-immigration) ambapo Vifaa vya kisasa vimefungwa ili kufanikisha upatikanaji wa huduma bora za Kiuhamiaji. 

Mfumo huu pia utawezesha kudhibiti mpaka huo kwa njia ya kielektroniki (e-Border Management Systems) suala ambalo litasaidia ulinzi na usalama.
Mfumo huu (e-Immigration) utatatua kero zinazosababishwa na urasimu usio wa lazima katika utoaji wa huduma za kiuhamiaji.













05 Oktoba 2019

“FANYENI KAZI KWA WELEDI NA KUZINGATIA SHERIA”, DKT. MAKAKALA


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala ametoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Idara ya Uhamiaji katika Mkoa wa Mbeya.

Akizungumza na Watumishi hao, Kamishna Jenerali amewasihi kujiepusha na vitendo vya rushwa na kufanya kazi kwa weledi na bidiii ili kwenda sambamba na kasi ya serikali ya Awamu ya Tano katika kuwaletea wananchi wake maendeleo na kukuza uchumi wa nchi yetu.

“Idara ya Uhamiaji ina jukumu kubwa la kukuza sekta za Utalii na Uwekezaji katika nchi yetu hivyo tunatakiwa kuwahudumia wageni wanaoingia na kuishi nchini bila vikwazo vinavyoweza kurudisha nyuma ustawi wa sekta hizo” amesitiza Dkt. Makakala.

Kwa upande wake Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya, Naibu Kamishna wa Uhamiaji Shaaban Omari ameeleza kuwa Idara inaendelea na mapambano dhidi ya Wahamiaji kwa kuwashirikisha Viongozi wa Serikali za Mitaa na Kata.

Viongozi hao Kata na Vijiji wanapatiwa Elimu ya Uhamiaji ili kuwajengea uelewa katika masuala ya Kiuhamiaji ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kutekeleza Mpango Mkakati wa Mapambano dhidi ya Wahamiaji haramu (Pekenyua Fukunyua) unaondelea nchi nzima kwa sasa.

Akiwa katika ziara hiyo Mkoani Mbeya, Dkt. Makakala ametembelea na kukagua Ofisi za Uhamiaji katika Vituo vya Uwanja wa Ndege wa Songwe pamoja na Mpaka wa Kasumulu.

Kesho Jumamosi Oktoba 5, 2019, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji atahudhuria Uzinduzi wa Kituo cha pamoja cha utoaji huduma za mpakani (OSBP) katika Mpaka wa Tunduma Mkoani Songwe ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akisalimiana na Maafisa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Uhamiaji Mkoa huo siku ya Alhamisi tarehe 04 Oktoba 2019 katika ziara ya kikazi mkoani humo.


Kaimu Mfawidhi wa kituo cha Uhamiaji Kasumulo akimuonesha Kamishna Jenerali wa Uhamiaji eneo litakalojengwa kityoo cha Mpaka wa Pamoja (OSBP).


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akiongea na raia wa DRC Bwana Jeane Pierre aliyekuwa akipata huduma za Uhamiaji katika mpaka wa Tunduma

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji pamoja na Kamishna wa Udhibiti na Usimamizi wa Mipaka wakiangalia ukamilishaji wa maandalizi ya ufunguzi wa kituo cha huduma za pamoja mpakani (OSBP) katika mpaka wa Tanzania na Zambia mji mdogo wa Tunduma. 

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akisaini kitabu cha wageni katika kituo cha Uhamiaji Tunduma mkoani Songwe