Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiongea na Watumishi katika Kituo cha Uhamiaji Tunduma mwishoni mwa wiki. |
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji
Dkt. Anna Peter Makakala amewaagiza Watumishi wa Idara ya Uhamiaji kufanya kazi
kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa wakati wanapotoa huduma kwa Wananchi
na raia wa kigeni.
Dkt. Makakala ametoa wito huo ikiwa ni Utekelezaji wa maagizo
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli aliyoyatoa wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Kituo cha Pamoja cha Huduma
Mpakani (One Stop Border Post - OSBP) cha Tunduma - Nakonde, tarehe Oktoba 5,
2019.
Awali Kamishna Jenerali alipokea
taarifa ya utendaji kazi wa kituo hicho na amewataka kuimarisha doria maeneo ya
mipakani na kushirikiana na watendaji kata na vijiji katika kuwabaini wahamiaji
haramu wanaojipenyeza na kuishi katika maeneo yao.
Idara ya Uhamiaji kama mdau wa
huduma mapakani hapo imeshiriki hafla uzinduzi wa Kituo hicho (Tunduma –
Nakonde OSBP) uliofanywa kwa pamoja na Marais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Jamhuri ya Zambia, Mhe. Edger Lungu.
Idara ya Uhamiaji imejipanga
kutoa huduma bora na za kisasa mpakani hapo kwa kutumia mfumo wa Uhamiaji
Mtandao (e-immigration) ambapo Vifaa vya kisasa vimefungwa ili kufanikisha
upatikanaji wa huduma bora za Kiuhamiaji.
Mfumo huu pia utawezesha kudhibiti
mpaka huo kwa njia ya kielektroniki (e-Border Management Systems) suala ambalo
litasaidia ulinzi na usalama.
Mfumo huu (e-Immigration) utatatua
kero zinazosababishwa na urasimu usio wa lazima katika utoaji wa huduma za
kiuhamiaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni