Kamishna Jenerali wa
Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala leo Jumatatu Oktoba 7, 2019 amewataka
Maafisa Uhamiaji Mikoa yote nchini kuimarisha Mapambano dhidi ya Wahamiaji
haramu.
Akizungumza na Watumishi wa
Uhamiaji Mkoa wa Rukwa (mjini Sumbawanga), Dkt. Makakala amesema kuwa nchi yetu
inaelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baadae Uchaguzi Mkuu. Hivyo
Maafisa Uhamiaji Mikoa yote nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi
hilo kwa kutoa Elimu kwa umma pamoja na kuhakikisha kuwa Wahamiaji haramu
hawashiriki zoezi hilo.
Kwa ushirikiano na Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, Idara ya Uhamiaji inatarajia kutoa Elimu ya Uraia kwa
kuanzia na Mikoa ya Kagera, Kigoma, Rukwa, Katavi na Geita. Maafisa Uhamiaji
wote nchini wametakiwa kuandaa vipindi maalum vyenye lengo la kuwajengea uwezo
na uzalendo wananchi hususan katika masuala ya Uraia.
“Kila
Mwananchi anao wajibu wa kulinda usalama wa nchi yetu kwa kutoa taarifa za
Wahamiaji haramu. Kumhifadhi au kumsaidia Mhamiaji haramu kupata kitambulisho
cha mpiga kura na kushiriki zoezi la kupiga kura kwa ama kuchagua au
kuchaguliwa ni kukosa uzalendo kwa nchi yetu” amesisitiza Dkt.
Makakala.
“Taifa
lolote Duniani liwe kubwa au dogo haliwezi kukamilika bila ya raia wake kwani
raia hao ndio wenye nchi na wanaotakiwa kunufaika na haki zitolewazo na
serikali kwa raia wake kwa mujibu wa katiba ya nchi ikiwa ni pamoja na haki ya
kuchagua au kuchaguliwa katika nafasi za uongozi Kwa upande mwingine ni raia
hao ndio wenye wajibu wa kulinda nchi yao” aliongeza Dkt.
Makakala.
Awali akitoa taarifa ya
Utendaji kazi katika Mkoa wa Rukwa, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Rukwa, Naibu
Kamishna wa Uhamiaji Elizeus Mshongi
ameeleza
kuwa mkoa wa Rukwa unapokea idadi kubwa ya wahamiaji haramu, wengi wao wanatoka
katika Mataifa ya Zambia, D.R Congo na Burundi.
Kwa kipindi cha cha kuanzia
Januari hadi Agosti, 2019; jumla ya wahamiaji haramu 128 wamekamatwa na
kuchukuliwa hatua mbalimbali ikiwamo kushitakiwa na kuondoshwa nchini.
Naibu Kamishna Mshongi
ameongeza kuwa Mkoa unaendesha zoezi la kuwatambua na kuwaorodhesha Wahamiaji
walowezi. Kupitia Zoezi hilo jumla ya Walowezi 5,743 wametambuliwa na
kuorodheshwa.
Aidha, Idara ya Uhamiaji
inatoa wito kwa Wahamiaji walowezi wote wanaoishi nchini kujitokeza na
kujiorodhesha, watakaoshindwa kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa
ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na kuondoshwa nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni