Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo leo
Jumanne Disemba 17, 2019 amefunga rasmi mafunzo ya Awali kwa askari wapya 400
wa Idara ya Uhamiaji, hafla ambayo imefanyika katika Chuo cha Uongozi cha Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT) Kimbiji mkoa wa Pwani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Jenerali Mabeyo amewataka Asakari
hao kufanya kazi kwa Uzalendo na kutii kiapo walichoapa leo kwa kutimiza
majukumu yao kwa weledi huku wakizingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za
Uhamiaji.
"Serikali imewaamini na kuwapatia dhamana kubwa hivyo kuweni
wazalendo na waadilifu wakati mnapowahudumia Wananchi"alisema Jenerali Mabeyo.
Pia Jenerali Mobeyo amempongeza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji
kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kufanya mabadiliko ndani ya Uhamiaji na
mahusiano mazuri yaliyopo na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, akitolea
mfano namna Idara ya Uhamiaji inavyoshughulikia maombi ya pasipoti kwa Maafisa
na Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanaokwenda nje ya
nchi kulinda amani.
Awali akimkaribisha Jenerali Mabeyo, Kamishna
Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala alimshukuru Jenerali Venance Mabeyo kwa
kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mafunzo hayo pamoja na kuwa anayo
majukumu mengi ya kitaifa.
Mafunzo hayo ya Awali kwa Askari wa Idara ya Uhamiaji ya Awamu
ya Kwanza kwa Mwaka huu yalifunguliwa tarehe 23 Septemba, 2019 na yamehitimishwa leo yamejumuisha Askari
wanaume 326 na wanawake 74.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni