Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni leo tarehe 18/12/2019 amehitimisha maadhimisho
ya Siku ya Kimataifa ya Wahamaji katika hafla iliyofanyika kwenye Viwanja vya Uhamiaji
Kurasini Dar Es Salaam. Maadhimisho hayo ambayo yanafanyika kila mwaka
yanalenga kutambua haki za wahamaji pamoja na familia zao wanapokuwepo katika
nchi za kigeni.
Akihutubia katika Maadhimisho
hayo Mheshimiwa Masauni amempongeza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala
kwa kufanya mabadiliko makubwa kwenye Mifumo ya kutolea huduma zake kwa njia ya
Mtandao ambapo sasa mgeni anaweza kuomba Visa au Vibali vya Ukaazi, kufanya
malipo pamoja na kupokea kibali chake kwa njia ya mtandao akiwa mahali popote
Ulimwenguni bila ya kulazimika kufika katika Ofisi za Uhamiaji.
Aidha, Naibu Waziri aliongeza
kuwa Serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji kwa kuanzisha vibali maalumu
vya ukaazi kwa wahamiaji walowezi walioo hapa nchini ili kutatua tatizo la
uhamiaji haramu nchini. Pia Serikali imepunguza ada ya kibali cha Ukaazi kwa
wawekezaji wan je wenye asili ya Tanzania (Diaspora) kutoka Dola za Kimarekani
3050 hadi kufikia Dola 1000 ili kuhamasisha raia hao kuwekeza katika nchi yao
ya asili.
Awali akimkaribisha Naibu Waziri
Masauni, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala ameeleza kuwa kwa
sasa Idara ya Uhamiaji inaendelea kuzifanyia kazi changamoto zinazo wakabili
wateja wa huduma za Uhamiaji.
Dkt. Makakala aliongeza kuwa
kutokana na maboresho hayo, Waombaji wa huduma za Uhamiaji hususani Pasipoti hawatalazimika kuwasilisha katika
Ofisi za Uhamiaji Viambata vya nakala halisi watakapo hitaji Pasipoti. Badala yake
Viambato hivyo vitatakiwa kuwasilishwa kwa njia ya Mtandao pekee.
Katika Maadhimisho hayo Idara
ya Uhamiaji na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) wamesaini
Makubaliano ambayo yatawezesha mifumo ya huduma ya Taasisi hizo mbili kupeana
taarifa muhimu ikiwemo cheti cha kuzaliwa ambacho ni mojawapo ya kiambata
muhimu wakati wa kuomba Pasipoti.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni