Matangazo

📢 IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA — KARIBU KWENYE BLOG RASMI   ✦   📰 UHAMIAJI HABARI BLOGU — TUNAKULETEA MATUKIO KILA SIKU   ✦   📲 FUATA IDARA YETU KATIKA MITANDAO YA KIJAMII   ✦   ✉️ WASILIANA NASI: info@immigration.go.tz   ✦   ☎️ +255-22-2850575/6

12 Machi 2020

Zaidi ya Maafisa na Askari 30 wa Jeshi la Uhamiaji Tanzania kutoka (JNIA) Wapatiwa Mafunzo Kabambe

Dar es salaam, Tanzania
Jeshi la Uhamiaji Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Canada imeendesha Mafunzo ya Kuwajengea uwezo Maafisa na askari wa Kituo cha Uhamiaji  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA)

Mafunzo hayo ya siku tatu yanahusisha jumla ya Maafisa na Askari 31 ambapo yanafanyika katika Ofisi ndogo za makao makuu ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar e salaam, na yanatarajiwa kumalizika kesho tarehe 13 Machi 2020.

Mafunzo hayo yana lengo kuu la kuwajengea uwezo mafisa na askari katika kutekeleza majukumu yao ya kuhudumia wageni na raia wa Tanzania katika vituo mbalimbali vya kuingia na kutoka nchini  sanjari na kudhibiti uingiaji wa Wahamiaji haramu.

Mafunzo hayo yameongozwa na Bwana David Henry kutoka ubalozi wa Canada nchini Tanzania ambapo Makao yake Makuu yapo Nairobi nchini Kenya.

Bwana Henry amefundisha mambo mbalimbali yanayohusu ukaguzi wa nyaraka mbalimbali za kiuhamiaji kwa kutumia njia mbalimbali za kisasa ili kuwabaini wahalifu wanaoweza kughushi nyaraka kama vile Pasipoti, Visa na Vibali vya ukaazi, sanjari na kufanya mahojiano kwa kina na mgeni au raia wa Tanzania kwa njia za kisasa zaidi wanapokuwa katika mipaka (Entry Points).

Mafunzo ya aina hii hutolewa mara kwa mara kwa maafisa na askari wa Uhamiaji Tanzania, chini ya kitengo cha mafunzo.

Aidha Mafunzo ya aina hii husaidia Maafisa na Askari kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, hasa katika kipindi hiki cha utekelezaji wa Uhamiaji Mtandao ambapo unaakisi mabadiliko ya kiteknolojia duniani ambayo yanakwenda kwa kasi na kutumia kiwango cha juu cha TEHAMA katika huduma mbalimbali na hatimae kuendana na utoaji wa huduma za kiuhamiaji zenye viwango vya kimataifa na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi na mipaka yake.  

HABARI PICHA NA MATUKIO
Baadhi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji kutoka Kituo cha (JNIA) Wakipatiwa mafunzo maalumu ya kujengewa uwezo

Bwana David Henry Mkufunzi kutoka Ubalozi wa Canada Nchini Tanzania akifundisha 

Baadhi ya Maafisa Uhamiaji wakifuatilia kwa makini mafunzo yanayotolewa na Bwana David Henry Kutoka Ubalozi wa Canada



Baadhi ya Maafisa Uhamiaji wakiangalia kwa makini moja ya kifaa cha kuchunguzia Pasipoti ili kutambua uhalali wake


Mafunzo yakiendelea kutolewa 

Picha ya Pamoja, Katikati ni Mkufunzi kutoka Ubalozi wa Canada Bwana David Henry na Kushoto kwake  ni Mratibu wa Mafunzo Mkaguzi wa Uhamiaji Nabwike Joseph wakiwa na Maafisa na Askari Waliopatiwa Mafunzo hivi karibuni

Mratibu wa Mafunzo Uhamiaji Mkaguzi Nabwike Joseph (Kushoto) akiagana na Mkufunzi Bwana David Henry Kutoka Ubalozi wa Canada (Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu).

10 Machi 2020

UHAMIAJI Tanzania Yatoa Mafunzo Kwa Mabalozi Wateule

Kamishna wa Uhamiaji anayesimamia Divisheni ya Vibali vya Ukaazi, Pasi na Visa, Mary Palmer (ndc) ameongoza Ujumbe wa Mabalozi 03 katika Mafunzo ya huduma mbalimbali za kiuhamiaji zinazotolewa katika Balozi za Tanzania Nje ya Nchi.

Waheshimiwa Mabalozi waliohudhuria mafunzo hayo ni Maj. Gen. Jacob Kingu, Kamishna Jenerali (Mstaafu) wa Magereza  Phaustine Kasike na Dkt. John Simbachawene ambao wameteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Katika mafunzo hayo, mada mbalimbali ziliweza kuwasilishwa na Maafisa kutoka Idara ya Uhamiaji hususani Pasipoti, Visa za kielektroniki, pamoja na Mifumo inayotumika katika utoaji wa Pasipoti na Visa za kieletroniki.

Aidha, Waheshimiwa Mabalozi walipata fursa ya kuuliza maswali na kujibiwa ipasavyo na watoa mada sanjari na kufurahishwa na namna mifumo mbalimbali ya Uhamiaji inavyofanya kazi  na kurahisisha utoaji wa huduma za uhamiaji kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa.

Kwa upande wake Balozi Mteule wa Tanzania Meja Jenerali Jacob Kingu kwa niaba ya mabalozi wenzake alimshukuru na Kumpongeza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kwa mafunzo waliyoyapata.

Pia ameongeza kuwa, mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kwenda kufanya kazi kwa ufanisi hususani katika kuwahudumia Watanzania waishio nje ya nchi na wageni wanaoingia hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo utalii, matembezi, Biashara na uwekezaji.

Mafunzo hayo Yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya  Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es salaam na ni muendelezo wa Elimu ya Uhamiaji na Uraia inayotolewa na Idara ya Uhamiaji kwa Makundi mbalimbali ikiwemo Wanadiplomasia.

 HABARI PICHA NA MATUKIO
Kamishna wa Uhamiaji anayesimamia Divisheni ya Vibali vya Ukaazi, Pasi na Visa, Mary Palmer (ndc) akitoa utangulizi wa Mafunzo kwa Mabalozi Wateule.


Balozi Mteule Maj. Gen. Jacob Kingu, akisikiliza kwa makini elimu anayopatiwa kutoka kwa Maafisa Uhamiaji



Mkaguzi wa Uhamiaji Gerald Kawishe akifundisha somo la Uraia na Pasipoti kwa Mabalozi wateule

Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji Godbless Swai akifundisha somo la Vibali vya Ukaazi na Visa kwa Mabalozi wateule (hawapo pichani)

Mabalozi wateule wakisoma kwa vitendo namna ya kukagua nyaraka mbalimbali za Kiuhamiaji
Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji  Ritha Muumba akifundisha Huduma za kibalozi (Consular Services) kwa Mabalozi wateule

Afisa TEHAMA Mwandamizi Rodern Mtulo Akisikiliza kwa makini maswali kutoka kwa mabalozi wateule baada ya kupata mafunzo ya Huduma za Kiuhamiaji


Picha ya Pamoja baada ya kumaliza Mafunzo
Mabalozi Wateule wakiagana baada ya kumaliza mafunzo katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya Uhamiaji  Kurasini Dar es salaam (Picha na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu)

09 Machi 2020

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara Afanya Ziara na Kugawa Vitendea kazi

Mtwara, Tanzania
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi James Mwanjotile amefanya ziara ya kikazi katika Wilaya zote za Mkoa wa Mtwara yaani Masasi, Newala, Nanyumbu na Tandahimba.

Lengo kuu la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiutendaji katika wilaya hizo na Mkoa kwa ujumla. 

Akizungumza na Maafisa, Askari na watumishi raia wa Uhamiaji katika Wilaya hizo, Kamishna Msaidizi Mwanjotile, amesisitiza kuhakikisha kuwa wanatunza vifaa vyote vya Ofisi pamoja na  kufanya kazi kwa weledi wakizingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali.

Aidha, amewakumbusha Maafisa Uhamiaji Wilaya kuendelea kutoa elimu kwa umma ambapo, Mkoa wa Mtwara tayari umeshaanza kuandaa programu maalum za Elimu ya Uhamiaji na Uraia kwa Umma kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, na kuhakikisha wanashughulikia changamoto za uraia zitakazo jitokeza wakati wa kipindi cha uchaguzi, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala alilolitoa hivi karibuni Jijini Dodoma.

Vilevile Kamishna Msaidizi Mwanjotile ametoa wito kwa Maafisa Uhamiaji Wilaya wote wa Mkoa huo kuhakikisha kuwa wageni wote wanaoishi katika maeneo yao wanafuata sheria, sanjari na kusisitiza kuongeza udhibiti wa uingiaji na utokaji wa wageni na raia wa Tanzania katika mipaka yote ya Mkoa huo kwa kuimairisha doria na misako ya wahamiaji haramu kote nchini ili kuhakikisha kuwa nchi inabaki salama na wahamiaji haramu hawanufaiki na rasilimali zetu.

HABARI PICHA NA MATUKIO 
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi James Mwanjotile akiwa katika moja ya Ofisi ya Uhamiaji Wilaya wakati wa ziara yake.




Baadhi ya vitendea kazi vikishushwa katika moja ya Wilaya za Mkoa wa Mtwara  (Picha zote na Ofisi ya Uhusiano Uhamiaji Mkoa wa Mtwara)

06 Machi 2020

UHAMIAJI Iringa Yatekeleza Agizo la Kamishina Jenerali wa Uhamiaji


Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Iringa imetekeleza agizo la Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala alilolitoa mapema wiki hii akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Dodoma kwa Maafisa Uhamiaji Mikoa yote nchini kutoa elimu ya Uhamiaji na Uraia kwa watanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020.

Akizungumzia kuhusu Utekelezaji huo, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Iringa Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Agness Luziga amesema Maafisa na Askari wa Uhamiaji Mkoa wa Iringa wanatembelea Maeneo mbalimbali Mkoani humo kwa ushirikiano na vyombo vya habari vikiwemo Vituo vya Radio, Televisheni na Mitandao ya Kijamii kutoa elimu ya Uhamiaji na Uraia hasa kuelekea kipindi hiki muhimu cha Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Kwa kushirikiana na Kituo cha Redio Furaha Fm 96.7 kilichopo katika Manispaa ya Iringa, wametoa elimu ya Uraia kwa Wananchi wa Mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla.

Kupitia Kipindi hicho Wananchi walipata fursa ya kuuliza maswali na kupatiwa ufafanuzi kuhusu huduma za Uhamiaji na Uraia.

Afisa Uhamiaji Mkoa huyo amesisitiza kuwa zoezi hilo ni endelevu na litashirikisha Viongozi wa Serikali za Mitaa, Tume ya Uchaguzi pamoja na Jamii kwa ujumla.


HABARI PICHA NA MATUKIO

Maafisa Uhamiaji Mkoa wa Iringa wakiwa ndani ya Kituo cha Redio Furaha Fm Kutekeleza Agizo la CGI la kutoa elimu kwa Umma kuhusu Huduma za Uhamiaji na Uraia katika Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020
(Picha zote na Ofisi ya Uhusiano Uhamiaji Mkoa wa Iringa)

05 Machi 2020

Ziara Ya Katibu Mkuu Mambo Ya Ndani: Uhamiaji Waaswa Kulinda Taswira Nzuri Ya Idara Yao


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ndg. Christopher Kadio amefanya ziara ya Kikazi Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu na kuzungumza na Menejimenti, Maafisa, Askari na Watumishi raia wa Uhamiaji alipofanya ziara ya kikazi Makao Makuu ya Uhamiaji - Dodoma, kwa lengo la kuona na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinaikabili Idara ya Uhamiaji na kuomba ushirikiano wa kutatua kwa pamoja.

Akizungumza na Watumishi hao, Katibu Mkuu Kadio amesisitiza utendaji kazi wenye kuzingatia weledi, nidhamu na unyenyekevu hasa wakati wa kupokea mrejesho wa huduma za Uhamiaji hususan kupitia malalamiko ama ukosoaji wa namna yoyote toka kwa watu Wananchi.

"Kupokea malalamiko na kuyafanyia kazi ni njia nzuri ya kutunza taswira ya taasisi na ama kulinda hadhi ya Idara yenu” amesisitiza 

Aidha, Katibu Mkuu amewataka watumishi hao kutoa maoni yao na ushauri kwa lengo kuboresha ufanisi wa Utendaji kazi.

Mtendaji Mkuu huyo wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi amesisitiza kuwa endapo Idara itafanikiwa kuzitatua changamoto zinazioikabili itakuwa ni Mafanikio kwa Wizara na Serikali kwa ujumla.

Pia Katibu Mkuu Kadio ameipongeza Idara kwa kuboresha kwa kiwango kikubwa utoaji wa huduma za Paspoti na kuwaasa kuwa kazi kubwa waliyonayo ni kulinda mafanikio hayo na kuendelea kuboresha zaidi ya ubora uliopo sasa.

Akihitimisha mazungumzo yake Ndugu Kadio ameahidi kukutana na watumishi mbalimbali walio chini ya Wizara na taasisi zake mara nyingi iwezekanavyo kwa lengo na kutatua changamoto zinazojitokeza na kuboresha zilizotatuliwa na kuongeza ubora zaidi.