Uhamiaji
Mtandao ni Nini?
Uhamiaji
Mtandao (e-Immigration) ni muunganiko wa Mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa
kufanya kazi kwa pamoja na kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za
kiuhamiaji.
Lengo la
Uhamiaji Mtandao
Lengo
kuu la Uhamiaji Mtandao ni Kuimarisha Ulinzi na Usalama wa Nchi yetu, Kudhibiti
ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kuimarisha utoaji wa huduma za kiuhamiaji
kwa raia na wageni wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali.
Mfumo
wa Uhamiaji Mtandao, utawezesha;
Idara ya Uhamiaji kutoa
viza kielektroniki (e-Visa); ambapo
mgeni ataweza kuwasilisha ombi lake na kupata majibu kwa njia ya kielektroniki.
Mfumo huo pia utasaidia Serikali kupata taarifa sahihi za malipo ya viza na
kuchagiza ukuaji wa Sekta ya Utalii nchini.
Mfumo wa Udhibiti na Usimamizi wa
Mipaka Kielektroni (e-Border Management), Mfumo
utasaidia kudhibiti na kuwezesha uingiaji na utokaji wa raia na wageni nchini,
Sambamba na hilo, Mfumo utasaidia kuchuja wageni wasiotakiwa kuingia nchini na hivyo
kuimarisha ulinzi hususan katika maeneo ya mipakani na kuzuia ongezeko la
wahamiaji haramu nchini.
Mfumo wa utoaji wa Vibali vya
Ukaazi Kielektroniki (e-Residence Permit), Mfumo huu
utasaidia kuboresha usimamizi wa utoaji vibali kwani mwombaji atawasilisha
maombi yake kwa njia ya kielektroniki. Hii itasaidia kukuza Sekta ya Uwekezaji
nchini kwa maendeleo ya uchumi wa Nchi yetu.
Mfumo wa Utoaji wa Pasipoti kielektroniki
(e-Passport); Mfumo huu ambao ndio wa kwanza katika
utekelezaji wa Mradi wa Uhamiaji Mtandao, utawawezesha waombaji wa huduma ya
Pasipoti kuwasilisha maombi yao kwa njia ya kielektroniki (Online Passport
Application) kutoka mahali popote walipo, na kuweza kufuatilia (Track) maombi hayo
kielektroniki.
Pasipoti
hii mpya ya Kielektroniki imesheheni sifa zifuatazo:
1. Imewekwa Kifaa maalum chenye uwezo
wa kutunza taarifa za mmiliki wa pasipoti “Micro-Chip” na hivyo kufanya suala
la utunzaji wa Usalama za Pasipoti hizi kuwa wa hali ya juu
2. Vile vile uwepo wa “Micro-Chip”
katika Pasipoti ya kielektroniki, kunaifanya pasipoti hii kuwa ngumu kuibiwa au
kutumiwa na wahalifu au watu wanaojaribu kuficha utambulisho
3. Vile vile
uwepo wa “Micro Chip” katika pasipoti ya kielektroniki, kunaifanya pasipoti ya
hii kuwa ngumu kuibiwa au kutumiwa na wahalifu au watu wanaojaribu kuficha
utambulisho wao kwa kutumia pasipoti zisizo zao.
4.
Pasipoti hiyo
ina viwango vilivyopendekezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Usafiri
wa Anga (ICAO).
5.
Pasipoti
inatumia mfumo bora wa Utunzaji wa taarifa za mmiliki wa Pasipoti
kielektroniki, ambao hurahisisha utunzaji wa taarifa za mhusika, na kuondoaa
urasimu wa ufuatiliaji wa kumbukumbu za mmiliki pale anapotaka huduma nyengine
6. Pasipoti
hiyo ina uwezo wa kutunza kumbukumbu za kibailojia (Biometric features)
Faida za Pasipoti Mpya ya Kielektroniki
Pasipoti
hii mpya ina uwezo wa kuhifadhiwa katika Simu ya Kisasa (Smart Phone) na hivyo
kumuwezesha mwenye nayo kupata msaada wa Hati ya Dharura katika Ubalozi wowote
wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pale anapopotelewa na
pasipoti hiyo awapo nje ya nchi ili aweze kurudi nyumbani.
Aidha, Pasipoti mpya ya Tanzania ya Kielektroniki ina muonekano
unaofanana na pasipoti za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na
faida zake ni nyingi;-
(i) Utambulisho wa
pamoja wa raia wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanapokuwa nchi
za nje na hivyo kurahisisha kupata msaada wa huduma za kikonsula (consular services)
inapobidi. Kwa mfano, kupata msaada wa kurejeshwa nchini kupitia balozi za nchi
wanachama wakati wa dharura, ikiwa sehemu husika haina ubalozi wa Tanzania.
(ii)
Raia
wa nchi wanachama kutambuana wanapokuwa nje ya nchi na hivyo kujenga umoja wa kikanda
kwa ngazi ya raia, wanapokuwa nje, kwani ni rahisi kupata msaada kwa jirani
kuliko mtu wa mbali.
|
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiweka saini yake kwenye kifaa cha kusaini cha kielektoniki kabla y akupatiwa pasipoti yake ya kielektroniki. |
|
Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akionesha pasipoti yake baada ya kukabidhiwa na Mheshimiwa waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Dkt. Mwigulu Mchemba. |
|
Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu akionesha pasipoti yake ya kielektroniki wakati wa uzinduzi wa pasipoti hizo kwenye Ofisi za Uhamiaji Makao Makuu, Kurasini jijini Dar es salaam. |