Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

01 Oktoba 2020

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala Atoa Elimu ya Uraia kwa Wamasai wa Ngorongoro Mkoani Arusha

Ngorongoro, Arusha

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Nchini (CGI) Dkt. Anna Makakala amefanya ziara ya Kikazi Wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha kukagua hali ya ulinzi na usalama wa mipaka ya Nchi na kuongea na wananchi wa Kijiji cha Enguserosambu kilichopo Wilaya ya Ngorongoro Mpakani mwa Kenya na Tanzania.

Akiongea na Wananchi wa Kijiji cha Enguserosambu mara baada ya kukagua mipaka na vipenyo vinavyotumika kupitisha Wahamiaji haramu CGI Dkt. Makakala amewataka Wananchi wanaoishi mipakani kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka yetu kwani suala la ulinzi ni Jukumu la kila Mwananchi.

CGI Dkt. Makakala aliendelea kuwaelimisha Wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro kuhusu masuala yote ya uraia wa Tanzania kwani Idara ya Uhamiaji ndicho chombo pekee kilichopewa mamlaka ya kutambua uraia wa mtu kwa mujibu wa sheria ya uraia Sura ya 357 rejeo la 2002.

“Idara itakuwa inapokea na kuzifanyia kazi taarifa zote zitakazotolewa kuhusiana na utata wa uraia wa mtu yeyote pasipo kujali dini, rangi, kabila au wadhifa wake katika jamii kwani inayo wajibu na mamlaka hayo kwa  mujibu wa kifungu cha 12(1)(d) cha Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 (Rejeo la 2016)” Alisema.

Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya Ngorongoro Mhe. Rashid Mfaume Taka amemshukuru Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala kwa kufika katika wilaya hiyo kwani ni viongozi wachache waliothubutu kufanya ziara za kikazi katika Wilaya hiyo na kufanya mkutano na Wananchi.

Aidha amemhakikishia Kamishna Jenerali kwamba Hali ya Ulinzi na Usalama katika Wilaya hiyo ni shwari na Wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida huku wakijiandaa kufanya Uchaguzi Mkuu wa Rais Wabunge na Madiwani kwa Amani na Utulivu.

Idara ya Uhamiaji Tanzania ilianzishwa chini ya kifungu cha 4 (1) cha Sheria ya Uhamiaji sura ya 54, Ikiwa ni moja ya chombo cha Ulinzi na Usalama chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, chenye wajibu mkubwa katika kuimarisha na kulinda usalama wa nchi, kwani moja ya majukumu yake ya msingi ni kuwezesha na kudhibiti uingiaji na utokaji wa watu pamoja na kusimamia ukaazi wa wageni Nchini.

Idara imeongeza udhibiti wa uingiaji na utokaji wa watu nchini, katika vituo vyote vya kuingia na kutoka nchini na pia imeongeza udhibiti katika vipenyo visivyokuwa rasmi ambayo hutumiwa na wahamiaji haramu kuingia nchini.

Lengo kuu likiwa ni kuhakikisha kuwa kila mtu anayeingia au kutoka nchini anapita katika vituo vinavyotambulika kwa mujibu wa sheria, ili kuweza kumtambua na pia kufahamu malengo yake ya kuja nchini na atakuwepo kwa muda gani hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi Mkuu sanjari na kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji, na vitongoji kubaini na kuwafichua wahamiaji haramu na walowezi waliopo nchini kinyume cha Sheria, kwa kutoa elimu ya uraia kwa viongozi hao.

Hata hivyo Idara imeendelea kufanya ukaguzi, Misako na Doria za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini kama vile nyumba za kulala wageni, viwandani, migodini, maeneo ya kazi, mipakani, vyombo vyote vya usafiri nk.

Ikumbukwe kuwa Utekelezaji wa shughuli zote za Idara ya Uhamiaji Tanzania ni kufikia Dira yetu ya Kuwezesha udhibiti wa uingiaji na utokaji wa watu nchini, kupitia utekelezaji wa sheria na kanuni zilizopo ili kulinda Usalama wa Taifa na kukuza Maendeleo ya Kiuchumi, sanjari na kutimiza Dhima ya kuwa taasisi yenye utendaji bora inayotoa huduma za Uhamiaji zenye kukidhi viwango vya kitaifa na Kimataifa, huku ikiongozwa na Motto wa “Uhamiaji, Usalama na Maendeleo”.

 HABARI PICHA NA MATUKIO

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Nchini (CGI) Dkt. Anna Makakala akiwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Ngorongoro tayari kwa ziara ya Kikazi Wilayani humo



Mkuu wa Wilaya Ngorongoro Mhe. Rashid Mfaume Taka akitoa Taarifa ya Hali ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala 

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji  Dkt. Anna Makakala akiwa Katika Picha ya Pamoja na Kamti ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngorongoro Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Rashid Mfaume Taka



Mkuu wa Wilaya Ngorongoro Mhe. Rashid Mfaume Taka (Katikati) akitoa maelezo ya Awali kwa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji  Dkt. Anna Makakala kuhusu Mpaka wa Kenya na Tanzania katika Kipenyo cha  Enguserosambu


 Kamishna Jenerali wa Uhamiaji  Dkt. Anna Makakala akiangalia (Beacon) inayotenganisha Mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo Wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha




Mtaalamu wa Mipaka Akitoa maelezo ya Mpaka kwa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji  Dkt. Anna Makakala





Kamishna Jenerali wa Uhamiaji  Dkt. Anna Makakala akisaini Kitabu cha Wageni katika Kijiji cha  Enguserosambu


Mkuu wa Wilaya Ngorongoro Mhe. Rashid Mfaume Taka Akiongea na Wananchi wa Kijiji cha Enguserosambu




Wananchi wa Kijiji cha Enguserosambu Wakimsikiliza kwa makini Kamishna Jenerali wa Uhamiaji  Dkt. Anna Makakala



(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni