Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

10 Julai 2020

CGI Dkt. Anna Peter Makakala atoa Maelekezo Haya Akiwa Ziarani Mkoani Tanga

Tanga,Tanzania
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania Dkt. Anna Makakala ameendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani Tanga ambapo mapema wiki hii alipokelewa kwa salamu ya heshima na Askari wa Uhamiaji Mkoa wa Tanga alipofika kwa ajili ya kufanya kikao kazi na Askari, Maofisa na watumishi raia wa Uhamiaji Mkoa wa Tanga.

CGI Dkt. Makakala amewataka Maofisa na Askari kuendelea kufanya kazi kwa utii uhodari uaminifu na weledi wa hali ya juu na kwa mujibu wa sheria kanuni taratibu na miongozo mbalimbali inayotolewa mara kwa mara na Idara.

Aidha ametoa maelekezo kwa Wilaya zote za Mkoa huo na Ofisi zote za Uhamiaji nchi nzima kuhakikisha hati zote za dharura (Emergence Travel Document) zinazotolewa, malipo yake yote lazima yafanyike kwa kutumia namba maalumu (Control Number) na si vinginevyo ili kurahisisha kukusanya maduhuli ya serikali.

Wakati huo huo amewakumbusha kuendelea kutimiza majukumu yao kwa weledi na kutojihusisha na rushwa na pia kuendel;ea kufanya doria za mara kwa mara na hatimae kudhibiti wimbi  la wahamiaji haramu wanaopita katika Mkoa wa Tanga.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi Afisa Uhamiaji Mkoa wa Tanga Mrakibu Mwandamizi Mbaraka Batenga amesema katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Kiuhamiaji, Mkoa una ofisi 11 za kutolea huduma za kiuhamiaji yaani Ofisi ya Mkoa, Ofisi za Wilaya ya Handendi, Pangani, Lushoto, Korogwe, Muheza, Kilindi na Mkinga, Kituo cha Horohoro, Uwanja wa ndege na Bandari.

Kazi zinazotekelezwa katika Mkoa huu ni pamoja na kutoa huduma za Pasipoti na hati nyingine za safari kwa watanzania wenye sifa, Kuhudumia raia wanaoingia na kutoka nje ya nchi, Kuratibu maombi ya wageni wanaoomba uraia wa Tanzania, kuanzia ngazi ya Kamati ya Usalama ya Kata hadi Mkoa na hatimaye kuyawasilisha katika Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu.

Shughuli nyingine ni pamoja na kufanya misako, doria na kuendesha mashtaka kwa makosa ya kiuhamiaji, kuratibu maombi ya hati za ukaazi kwa wageni wanaokidhi matakwa ya sheria ya kuishi nchini kwa madhumuni mbalimbali, kukusanya maduhuli ya serikali yanayotokana na malipo mbalimbali ya huduma za kiuhamiaji, Kuidhinisha maombi ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) Kwa wenye sifa na pia kuwatambua na kuwaorodhesha wahamiaji walowezi.

Shughuli za Uhamiaji katika ngazi ya Kata zimeimarishwa ambapo kila Afisa /Askari amepangiwa eneo la Kata kwa ajili ya kushirikiana na viongozi waliopo kufuatilia shughuli zote za kiuhamiaji katika Kata husika.

“Utekelezaji wa shughuli zetu katika Kata kwa kiasi kikubwa unaturahisishia kupata taarifa katika ngazi ya kitongoji, kijiji au mtaa na kufanyia kazi haraka” alisema SSI Batenga Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Tanga.

Kutokana na sababu za kihistoria na kijiografia Mkoa wa Tanga umekuwa na muingiliano mkubwa wa wageni hususani kutoka nchini Kenya,India, nchi za Uarabuni, Msumbiji, Burundi na Kongo hivyo Mkoa huo unaweza kuchukuliwa kuwa ni Mkoa ambao ni cosmopolitan katika masuala ya Uhamiaji
HABARI PICHA NA MATUKIO
Baadhi ya Maofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Tanga Wakijiandaa kumpokea Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania Dkt. Anna Makakala akiwa katika sehemu maalumu (Saluting Base) ya kupokelea salamu ya heshima utoka kwa askari wa Uhamiaji (Hawapo pichani)






Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania Dkt. Anna Makakala akisaini kitabu cha wageni Katika Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Tanga









Picha ya Pamoja ya Askari wapya Uhamiaji Baada ya kumaliza Kikao na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania Dkt. Anna Makakala Mkoani Tanga (Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Makao Makuu)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni