Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

07 Julai 2020

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala Aipongeza Uhamiaji Tanga kwa Juhudi za Kupambana na Wahamiaji Haramu

Tanga, Tanzania

Moja ya matatizo yanayolikabili Taifa letu pamoja na Mataifa mengine, ni tatizo la Wahamiaji haramu, tatizo hili kwa sasa ni ajenda ya Kitaifa na kimataifa kutokana na ongezeko la wimbi la wahamiaji haramu katika maeneo mbalimbali nchini na duniani kwa ujumla.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiwa ziarani Mkoani Tanga ameipongea Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Tanga na vyombo vingine vya vya Ulinzi na Usalama vya mkoa huo chini ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela kwa kuendelea kushirikiana na Idara ya Uhamiaji Mkoa katika kupambana na Kudhibiti Uhamiaji haramu.

Ameyasema hayo mapema leo hii wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Tanga ambapo ametembelea na kukagua utendaji kazi wa askari na maofisa uhamiaji katika vituo mbalimbali vya uhamiaji vilivyopo mkoani Tanga ikiwemo Ofisi ya Afisa Uhamiaji Wilaya ya Mkinga, Mpaka wa Kenya na Tanzania (Horohoro OSBP) pamoja na vipenyo vyake vya Kijiji cha Jasini sanjali na kukagua hali ya ulinzi na usalama wa mipaka.

  
Akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Jasini Kilichopo Wilaya ya Mkinga ambacho ni moja ya kipenyo cha kupitishia wahamiaji haramu, Dkt. Makakala amewataka Wananchi hao kuwa walinzi namba moja na kuacha tabia ya kupitisha wahamiaji haramu kwani kwa kufanya hivyo kunahatarisha ulinzi na usalama wa Taifa.
  

Wakati huo huo Dkt. Makakala ameongea pia na Wananchi wa kijiji cha Moha Kilichopo Wilaya ya Mkinga ambacho nacho hutumika kama kipenyo cha kusafirishia wahamiaji haramu na kuwahakikishia kwamba Uhamiaji na Wananchi washirikiane katika kuwafichua wahamiaji haramu na pia ametoa maelekezo kwa uongozi wa Mkoa na Wilaya kuendelea na doria za mara kwa mara.
  

Akitoa taarifa ya Utendaji kazi ya Mkoa Afisa Uhamiaji Mkoa wa Tanga Mrakibu Mwandamizi  Mbaraka Batenga alisema, Katika Kipindi cha Mwezi Januari hadi Juni mwaka huu 2020, imefanyika doria na misako mbalimbali ambapo watuhumiwa 123 walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa Mahakamani, Mashauri yaliyofikishwa mahakamani ni 20, kesi zinazoendelea 04 na wafungwa 76
  


Baadhi ya sababu zinazochangia kuwepo  kwa wahamiaji haramu ni kwamba, Tanzania kwa muda mrefu imekuwa kimbilio la wageni wanaotafuta hifadhi ya ukimbizi kutokana na machafuko ya kisiasa na kijamii katika nchi zao.
 


“Baadhi yao wamekuwa hawafuati taratibu za kuishi hapa nchini kama wageni halali, Aidha wengine walikwepa zoezi la kurejea kwao kwa hiari yao na pia hawakuhalalisha ukaazi wao nchini na hivyo kuendelea kuishi kinyume cha sheria” alisema.
  

Amani na Utulivu wa nchi yetu vimepelekea raia wa nchi jirani pamoja na nchi nyingine ambazo zimekuwa zikikumbwa na matatizo ya ndani ikiwemo vita ya wenyewe kwa wenyewe  kuifanya Tanzania kimbilio lao na baadhi yao kuishi nchini kinyume cha sheria .
  

Mfano, wimbi la Wasomali na Waethiopia wanaokamatwa mara kwa mara kwa kuingia nchini kinyume cha sheria.
  

Upo uhusiano pia wa kijamii hasa katika maeneo ya mipakani, hivyo kuwepo na uhusiano wa ndoa (Intermarriages) kati ya Watanzania na wageni wenye Imani potofu kwamba kuoa au kuolewa tu na kupata cheti cha ndoa kunampa mgeni uhalali wa kuishi nchini bila hati yoyote kutoka Idara ya Uhamiaji.
  

Dkt. Makakala ameeleza pia namna Idara ya Uhamiaji ilivyojipanga kuendelea kukomesha vitendo vya uhamiaji haramu kupitia kitengo maalumu cha utawala wa mipaka na Operesheni (Border Management and Operations) ili kuimarisha udhibiti wa mipaka, misako, doria na shughuli za operesheni
  

Mbali na hilo Idara imeanzisha daftari maalumu la kuandikishia wageni katika Mikoa mbalimbali hususani ile ya mipakani. Idara imekuwa ikitoa elimu kwa umma ili kuwaelimisha wananchi madhara ya kuwakumbatia wageni ambao hawana vibali vya kuishi nchini.
  

Aidha katika ziara hiyo Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala alifanya kikao na watumishi wa Mkoa wa Tanga na kusisitiza Upendo, Nidhamu, Utii, Ushirikiano na Kukataa rushwa na kutoa maelekezo ya kuhakikisha kuwa suala la wahamiaji haramu linadhibitiwa kabisa
 

Mhamiaji Haramu ni Raia wa kigeni anayeingia nchini na kuendelea kuishi kinyume na sheria za uhamiaji, au anayeingia nchini kwa mujibu wa sheria za uhamiaji, lakini akaendelea kuishi nchini kinyume na sheria, kanuni na taratibu husika.



HABARI PICHA NA MATUKIO
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiwa akisaini Kitabu cha wageni Mkoani Tanga alipokutana na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo na kufanya nayo mazungumzo
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala wa Kwanza Kulia akifanya mazungumzo na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Tanga
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiwa katika Picha ya Pamoja na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tanga alipowasili kwa safari ya kikazi
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akisalimiana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Mkinga alipofika ofisini hapo kwa ziara ya kikazi



Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akisaini Kitabu cha wageni katika Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya kikazi
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akisalimiana na Maofisa Uhamiaji na baadhi ya Watumishi wa taasisi mbalimbali zilizopo katika Mpaka wa Kenya na Tanzania Horohoro (OSBP) Mkoani Tanga Tanga wakati wa ziara yake ya Kikazi


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiwasikiliza Maofisa, askari na Watumishi raia wa Uhamiaji alipofanya kikao katika Kituo cha Mpaka wa Horohoro


Mfawidhi wa Kituo cha Mpaka wa Horohoro Mrakibu wa Uhamiaji Malisa akiwa katika kikao cha Kamishna Jenerali wa Uhamiaji na Maofisa na askari wa Kituo hicho


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiwasili katika Kijiji cha Jasini kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akisalimiana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Jasini alipowasili kwa ajili ya ziara yake ya kikazi





Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akioneshwa moja ya (Beacon) ya Mpaka kati ya Kenya na Tanzania uliopo katika  Kijiji cha Jasini Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiwa tayari kuongea na wananchi wa Kijiji cha Jasini Tanga


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiongea na wanachi wa Kijiji cha Jasini Kuhusu namna ya Kushirikiana na  serikali kwa ajili ya kudhibiti wahamiaji haramu.




Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akikagua moja ya bandari bubu ya Moa iliyopo wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga ambayo hutumika kupitishia Wahamiaji Haramu


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiongea na mwenyeji wa Kijiji cha Moa, (katikati) ni Afisa Uhamiaji Mkoa wa Tanga Mrakibu Mwandamizi Mbaraka Batenga





Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiongea  wananchi wa kijiji cha Moa, kulia kwake aliyekaa ni Mwenyekiti wa Kijiji

(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni