Kamishna Jenerali wa
Idara ya Uhamiaji (CGI) Dkt. Anna Makakala amefanya ziara ya kikazi katika
mpaka wa Holili OSBP unaotenganisha nchi ya Kenya na Tanzania Uliopo katika
Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro ili kukagua hali ya ulinzi na usalama wa
mipaka na utendaji kazi wa maofisa na Askari wa Uhamiaji hasa katika kipindi hiki cha
kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais Wabunge na Madiwani.
Akiongea na Maofisa,
Askari na Watumishi mbalimbali wa Taasisi nyingine za serikali zilizopo katika
mpaka huo amewataka kuendeleza ushirikiano uliopo na kuwa na umoja ili
kufanikisha ulinzi na usalama wa mpaka kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa na
kizazi cha sasa na baadae.
“Mpaka haulindwi na mtu mmoja unalindwa kwa ushirikiano na kufanya kazi
kwa pamoja, kwani kufanya hivyo ndio nguzo kubwa na muhimu ya kufikia mafanikio yetu kama
nchi, pia tuendelee kukemea rushwa na kutojihusisha nayo kabisa kwani Rushwa ni
Adui wa haki na inaweza kuliangamiza Taifa” Alisema CGI Dkt. Makakala
Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu CGI Dkt. Anna Makakala ametoa rai kwa wananchi wote wanaoishi mipakani kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kutoa taarifa pale wanapoona wageni wasiowatambua sanjari na kuwa walinzi namba moja kwani jukumu la ulinzi na usalama wa nchi ni jukumu letu sote.
Kwa upande wake Afisa
Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACI) Tununasya Ng’ondya
amemuomba Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kuweza kuanzishwa kwa Ofisi ya Uhamiaji
Wilaya ya Rombo ili kusaidiana na Vituo vya Uhamiaji vya Holili na Tarakea
kuweza kudhibiti wahamiaji haramu na kusogeza zaidi huduma nyingine za
Kiuhamiaji karibu na wanachi zaidi
Akitoa taarifa ya hali ya Mpaka Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji Holili (OSBP)Mrakibu Michael Mtuba amesema hali ya ulinzi na usalama mpakani hapo ni shwari na wamejipanga vilivyo kuendelea kutimiza majukumu yao kwa uhodari na weledi wa hali ya juu huku wakishirikiana kwa karibu sana na taasisi zote zinazofanya kazi katika mpaka huo.
Ziara ya CGI Dkt. Anna Makakala ilianzia katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Rombo ambapo alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya na kufanya nayo mazungumzo juu ya namna ya kuendelea kulinda mipaka ya nchi yetu na kutokomeza kabisa uingiaji wa wahamiaji haramu katika vipenyo mbalimbali vilivyopo katika Wilaya hiyo ya Rombo.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI) Dkt. Anna Makakala akisalimiana na Watumishi wa TRA alipofanya ziara ya kikazi katika mpaka wa Holili OSBP hivi Karibuni |
Baadhi ya Maofisa na Askari wa Uhamiaji wa Kituo cha Holili |
Baadhi ya Maofisa wa Taasisi Mbalimbali zilizopo katika Kituo cha Holili OSBP Wakimsikiliza kwa Makini Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala alipofanya ziara mpakani hapo hivi karibuni |
Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji (CGI) Dkt. Anna Makakala akisaini kitabu cha wageni katika Kituo cha Uhamiaji Holili OSBP |
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Naibu Kamishna Abdallah Towo akimsikiliza kwa Makini CGI Dkt. Anna Makakala wakati wa Kikao na Maofisa na Askari katika Kituo cha Uhamiaji Holili |
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACI) Tununasya Ng'ondya |
Muonekano wa Jengo la Holili OSBP |
Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji (CGI) Dkt. Anna Makakala akiwa katika Picha ya Pamoja |
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI) Dkt. Anna Makakala akisalimiana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Rombo |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni