Mwanga, Kilimanjaro
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji CGI Dkt. Anna Makakala amefanya ziara ya kikazi Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro na kufanya ukaguzi wa Mipaka na vipenyo vinavyopitisha wahamiaji haramu.
Akiwa Wilayani humo CGI Dkt. Anna Makakala ameafanya ukaguzi wa kipenyo cha Kitobo kilichopo katika Kitongoji cha Munoa Kata ya Kileo Tarafa ya Kitobo Wilayani Mwanga ambapo wananchi wa eneo hilo wameomba kufunguliwa kwa kituo cha kutolea huduma za Kiuhamiaji kutokana na Mwingiliano wa karibu uliopo wa wananchi wa Kenya na Tanzania katika eneo hilo.
Akijibu ombi la wananchi hao CGI Dkt. Anna Makakala amewaambia wananchi wa eneo hilo kwamba suala lao amelichukua na atalifikisha katika eneo husika ili lijadiliwe na ni lazima kuwe na makubaliano baina ya nchi mbili husika hivyo kutokanana na mwingiliano mkubwa na shughuli za kiuchumi za eneo hilo kuna haj asana ya kuanzisha kituo cha huduma za kiuhamiaji na huduma nyingine kama vile TBS, TRA na wadau wengine wa Mipakani.
CGI Dkt. Makakala pia ametembelea maeneo mengine ya Vipenyo vya kupitisha wahamiaji haramu vikiwemo kipenyo cha Kitohoto kilichopo kata ya Kivisini Tarafa ya Jipende na Kipenyo cha Mkisha Wilayani Mwanga.
Aidha ameishukuru kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Mwanga ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Thomas Cornel Apson kwa kuwa na ushirikiano mkubwa katika kupambana na wahamiaji haramu huku akitoa wito kwa wananchi kushirikiana na kutoa taarifa pale wanapoona wageni ambao hawawafahamu kutoa tarifa kwa viongozi na hatua zichukuliwe haraka sana, kwani suala la ulinzi na usalama wa nchi yetu ni jukumu letu sote .
Kwa upande wake Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACI) Tununasya Ng’ondya alisema Idara ya Uhamiaji Mkoa imendelea kufanya doria na misako ya mara kwa mara katika maeneo mengi ya wilaya ya Mwanga ili kudhibiti wimbi la Wahamiaji haramu hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi Mkuu wa Rais Wabunge na Madiwani ili kuhakikisha hali ya Ulinzi na Usalama mpakani hapo unakuwa shwari.
Afisa Uhamiaji Wilaya ya Mwanga Mrakibu Lydia Moshi alimshukuru Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania Dkt. Anna Makakala kwa kufika katika maeneo hayo yenye changamoto za uingiaji wa wahamiaji haramu ili kujionea hali halisi na namna wilaya ya Mwanga inavyotekeleza majukumu yake kwa weledi na uhodari wa hali ya juu katika kupambana na Wahamiaji Haramu katika maeneo yao ili kuhakikisha nchi na mipaka inakuwa salama wakati wote.
Ziara ya CGI Dkt. Anna Makakala ni muendelezo wa Ziara zake za Kikazi ambapo anakagua Mipaka na utendaji kazi wa Maafisa na Askari wa Uhamiaji nchini.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji CGI Dkt. Anna Makakala akitoa maelekezo kwa Maafisa Uhamiaji wakati wa ziara yake ya Kikazi Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro hivi karibuni |
Ukaguzi Ukiendelea |
Afisa Uhamiaji Wilaya ya Mwanga Mrakibu Lydia Moshi |
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Munoa Bw. Ridhiwan Ismail akimuonesha Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania Dkt. Anna Makakala njia nyingine zisizo rasmi ambazo hutumiwa na Wahamiaji haramu kuvuka |
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji CGI Dkt. Anna Makakala akisisitiza jambo |
Maeneo wanakopita wahamiaji haramu yakioneshwa |
(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu) |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni