Dar es salaam
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI) Dkt. Anna Makakala mapema wiki hii amefanya ziara ya kikazi katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es salaam na kufanya kikao na Maafisa na Askari wa Uhamiaji katika Kituo hicho.
Akiongea uwanjani hapo CGI Dkt. Makakala amesema kwamba Idara ya Uhamiaji iko macho muda wote katika ulinzi wa mipaka yote ya nchi ikiwemo katika uwanja huo ambao ni lango la kuingilia nchini (Entry Point)
“Zingatieni Maadili na Misingi ya kazi yenu, huku mkiongeza Umakini Uhodari Uaminifu na Weledi katika kutoa huduma za kiuhamiaji zenye viwango vya kitaifa na kimataifa sanjari na kuendelea na juhudi za Ulinzi na Usalama hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais Wabunge na Madiwani” alisema
Aidha amewakumbusha Maofisa na Askari kuendelea kuishi katika kauli mbiu ya Uhamiaji yenye Upendo Mshikamano Uwajibikaji na Kukataa Rushwa, ili kuwezesha kudhibiti uingiaji na utokaji wa watu kupitia utekelezaji wa sheria na kanuni zilizopo ili kulinda Usalama wa Taifa na kukuza Maendeleo ya Kiuchumi.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhamiaji Uraia na Pasipoti Gerald Kihinga amewaeleza pia Maafisa na askari juu ya maendeleo mazuri ya Ujenzi wa chuo cha Uhamiaji Kinachojengwa huko Wilayani Mkinga Mkoani Tanga ambapo amemshukuru Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala kwa kuwa na dira ya kuanzisha chuo hicho kwa ajili ya mafunzo ya Maafisa na Askari kwa ngazi zote.
Mfawidhi Mkuu wa Kituo cha Uhamiaji Katika Uwanja huo Naibu Kamishna wa Uhamiaji DCI Albert Rwelamira amemhakikishia Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala kwamba wataendelea kutoa huduma zenye kiwango cha kitaifa na Kimataifa kwa utii uhodari, uzalendo na weledi wa hali ya juu ili kufikia malengo ya Idara na Taifa kwa ujumla.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini CGI Dkt. Anna Makakala |
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI) Dkt. Anna Makakala Akiongea na Maofisa na Askari wa Kituo cha Uhamiaji cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa (JNIA) |
Baadhi ya Maafisa na Askari wakimsikiliza kwa Makini Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI) Dkt. Anna Makakala |
Askari wa Uhamiaji JNIA |
(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu ) |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni