Idara ya Uhamiaji inashiriki katika Maonesho ya 15 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Rock City Mall, Mwanza kuanzia tarehe 28 Agosti hadi tarehe 6 Septemba 2020.
Maonesho hayo yenye kauli mbiu 'Maendeleo ya Viwanda na biashara katika kukuza Ajira Nchini', yalifunguliwa rasmi tarehe 1 Septemba 2020 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na biashara Mhe. Innocent Bashungwa.
Maonesho haya yameandaliwa na Tanzania Chamber of Commerce, Industry and Agriculture (TCCIA) ambapo kwa mwaka huu washiriki kutoka nje ya nchi hususan nchi za EAC wameshindwa kuhudhuria kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19.
Rais wa TCCIA alisema kuwa bado kuna changamoto ya vikwazo vya biashara visivyo vya kikodi (Non-Tariff Barriers -NTBs), na taratibu za mpakani zinazokwamisha biashara ambapo aliiomba serikali ishughulikie pamoja na nchi wanachama wa EAC ili kurahisisha ufanyaji wa biashara katika nchi za jumuiya ya EAC ambapo Serikali imesema tayari ilishaanza kushughulikia changamo hizo nakuzitafutia ufumbuzi.
Idara ya Uhamiaji kwa upande wake inashiriki maonesho haya kwa kutoa elimu kwa wananchi na raia wa kigeni wanaofika katika banda lake. Naibu Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Edward Mbaku alisema kuwa mwitikio wa wananchi kutembelea banda la uhamiaji ni mkubwa ambapo maswali mengi kuhusu taratibu za Maombi ya Pasipoti, Uraia wa Tanzania na Vibali vya Ukaazi yamekuwa yakiongoza kwa kuulizwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni