Rombo, Kilimanjaro
Washiriki wa mafunzo ya Masuala ya Kiuhamiaji yaliyofanyika katika Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) kutoka katika Taasisi mbalimbali nchini wametembelea kituo cha pamoja cha mpakani Holili OSBP katika mpaka wa Kenya na Tanzania uliopo Wilayani Rombo Mkoani Kilimanjaro na kupongeza namna serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyojipanga katika kuwahudumia wageni na raia wa Tanzania kwa viwango vya Kimataifa.
Akitoa elimu kwa washiriki juu ya namna mpaka unavyofanya kazi katika Kituo hicho cha pamoja, Mfawidhi wa Kituo cha Holili OSBP Mrakibu Michael Mtoba amesema kwamba kituo hicho ndio kituo cha kwanza kabisa kuanzishwa katika vituo vya pamoja hapa nchini.
“Kituo hiki ndicho kituo cha kwanza kabisa kuanzishwa, kwani kilianzishwa Februari 2016 halafu vingine ndio vikafuata na nchi nzima mpaka sasa tuna vituo vya pamoja mpakani yaani OSBP zaidi ya saba ambavyo baadhi yake ni kama vile kituo cha Namanga, Horohoro, Sirali, Rusumo, Tunduma nk. alisema Mrakibu Mtoba.
Uendeshaji wa OSBP Unaongozwa na sheria ya OSBP ya mwaka 2015 ambayo inatamka uanzishwaji wa OSBP Katika nchi ya Tanzania, lakini pia ipo sheria ya Afrika Mashariki ya OSBP ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2017 ambazo zinaongoza namna ya kufanya kazi mpakani baina ya nchi husika katika OSBP.
Kwa pande wake Afisa Forodha wa Kituo cha OSBP Holili kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Moses Mwankenjela aliwaeleza washiriki wa mafunzo kutoka TRITA Namna Utaratibu huu wa mfumo wa pamoja mpakani unavyokuwa na faida kubwa katika utendaji kazi ikiwemo ukusanyaji wa mapato ya nchi na kurahisisha kufanya kazi na kuhudumia wananchi na wageni kwa wingi, wakati uhodari na kwa weledi wa hali ya juu.
Aidha ameeleza kwamba TRA na Uhamiaji wamekuwa wakishirikiana sana katika kuendesha shughuli za hapo mpakani huku wakishirikiana kikamilifu na taasisi nyingine za serikali zinzofanya kazi mpakani bila kusahau vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha mpaka unakuwa salama wakati wote kwa manufaa ya Wananchi wa kizazi cha sasa na baadae sanjari na kuleta maendeleo ya taifa.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo ya masuala ya kiuhamiaji kutoka katika taasisi mbalimbali wameipongeza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Idara ya Uhamiaji kwa kuwa na mifumo imara mipakani na kutoa huduma za kiuhamiaji zenye viwango vya kitaifa na kimataifa hasa ule wa Uhamiaji Mtandao ambao huleta faida nyingi kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tulikwenda leo Holili mpakani kwa kweli tumeona jinsi ambavyo taasisi za serikali zinavyofanya kazi vizuri mpakani na maelezo yao yametusaidia sana katika kujifunza mengi na tunaipongeza sana serikali, pale Holili wanafanya kazi vizuri sana alisema mmoja wa washiriki Bw. Cletus Majani.
Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Kilichopo Moshi Mkoani Kilimanjaro kinaendesha mafunzo ya usimamizi wa masuala ya kiuhamiaji kwa wadau wa masuala ya Kiuhamiaji nchini, na hushirikisha maafisa watendaji na wamiliki wa biashara mbalimbali zinazohudumia wageni ama kuajiri wageni au kufanya biashara na wageni.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Washiriki wa mafunzo ya Masuala ya Kiuhamiaji Wakifurahia jambo baada ya Kutembelea Mpaka wa Pamoja wa Tanzania na Kenya Holili OSBP |
Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji Holili OSBP aliyenyoosha mkono Mrakibu Michael Mtoba akionesha mpaka wa Tanzania na Kenya unapoishia |
Mkufunzi kutoka TRITA Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Shaibu Mbwilo akimuonesha mmoja wa Washiriki eneo linalotenganisha mpaka wa kenya na Tanzania |
Washiriki wa Mafunzo wakiongalia moja ya (Beacon) inayotenganisha Kenya na Tanzania katika eneo la Holili Wilayani Rombo Mkoani Kilimanjaro |
Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji Holili OSBP Mrakibu Michael Mtoba akiongea na Washiriki wa mafunzo hawapo Pichani |
Afisa Forodha wa Kituo cha OSBP Holili kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Moses Mwankenjela akiwaeleza Washiriki wa mafunzo namna TRA Inavyoshirikiana na Uhamiaji pamoja na Taasisi nyingine Mpakani |
(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Makao Makuu ya Uhamiaji) |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni