Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

21 Desemba 2020

Waziri Simbachawene Atoa Rai kwa Wananchi Kudumisha Amani, Umoja na Mshikamano.

Dodoma

Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene ametoa wito kwa wanachi wa Tanzania kuendelea kudumisha Amani, Umoja na Mshikamano kwa raia wa kigeni  wanaoishi hapa Nchini kihalali bila kuwabagua kutokana na dini au rangi yao kama ilivyoasisiwa na Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere.

Ameyasema hayo wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wahamaji Duniani (International 

Migrants’ Day), ambayo huadhimishwa Disemba 18 ya kila mwaka.

Maadhimisho hayo Kitaifa yalifanyika Jijini Dodoma katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere huku yakiongozwa na Kauli Mbiu ya mwaka huu isemayo:- ‘Reimagining Human Mobility’ yaani “Mtazamo Mpya wa Uhamaji wa Watu.”  

Aidha Mhe. Waziri amewataka wazazi na walezi kuwalinda watoto wao hasa mabinti wa umri wa kati ili wasijihusishe na mawakala au watu wenye nia ovu ya kuwasafirisha nje ya nchi kwa ahadi za kuwatafutia ajira wakati wanaenda kuteseka.

Hata hivyo ametoa rai kwa raia wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi kuwa mabalozi wazuri kwa kuishi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za uhamiaji kwa  nchi husika, sanjari na kutambua umuhimu wa wao kuja na kukumbuka kwao, kuwekeza na kutambua umuhimu wa kazi nzuri zinazofanywa na  serikali iliyopo madarakani.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Nchini (CGI) Dkt. Anna Makakala akitoa maelezo ya siku hiyo kwa waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alisema Mataifa mbalimbali duniani yanatambua mchango wa wahamaji katika kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wa Idara ya Uhamiaji  imeendelea kutoa huduma za Pasipoti na Hati za kusafiria kwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa ili kuwawezesha kusafiri nje ya nchi kwa madhumuni mbalimbali kama masomo, ajira, biashara au kutafuta fursa za kiuchumi.

“Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, jumla ya raia wa Tanzania 115,980 wamepatiwa Pasipoti Mpya za Kielektroniki kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Novemba, 2020, Huu ni mtazamo mpya katika kuwawezesha raia wa Tanzania kutafuta fursa mbalimbali za maendeleo duniani, na hivyo kufikia kauli mbiu hii” Alisema Dkt. Makakala.

Pia Idara imeendelea kutoa vibali vya ukaazi, pasi na viza za kielektroniki kwa raia wa kigeni wanaokuja kuishi hapa nchini na kufanya shughuli mbalimbali kama vile Uwekezaji, Utalii, Ajira, Masomo au shughuli zingine zinazotambulika kisheria.

Aidha, kumekuwepo na mazingira rafiki ya kuomba na kupata viza na vibali kwa raia wa kigeni, Uwezeshaji huu hutolewa kwa watu wenye sifa ya kuingia nchini pekee.

CGI Dkt. Anna Makakala aliendelea kueleza kwamba, kundi hilo la wageni, ni muhimu sana katika maendeleo ya kiuchumi kwani huchangia katika pato la Taifa, Katika kipindi cha Januari hadi Novemba, 2020, jumla ya raia wa kigeni 198, 873 wamepatiwa visa za Kielektroniki na wengine 8,308 wamepatiwa Vibali vya Ukaazi vya Kielektroniki.

Hatua hii, imewezesha mazingira bora ya utalii, biashara, uwekezaji, na kurahisisha uhamaji kwa raia wa kigeni kwa njia salama na kwa utaratibu (safely and orderly manner) ili kufanikisha mtazamo mpya wa uhamaji wa watu kwa maendeleo.

Sambamba na kuwezesha uhamaji, Idara ya Uhamiaji imeweka kipaumbele katika eneo la usalama, ambapo kwa wageni wasio kidhi vigezo vya kuingia nchini Idara imeendelea kuimarisha udhibiti wa uingiaji na utokaji wa watu, hatua hii ni muhimu sana kwani pasipo kuwa na amani na usalama ni vigumu kufanya shughuli za maendeleo ya kiuchumi.

Katika kulinda usalama wa nchi yetu, Idara imeendelea kuimarisha mifumo yake ya utendaji ili kuhakikisha kwamba uingiaji, utokaji na ukaazi wa watu hapa nchini ni salama.

Katika jitihada za kuimarisha usalama wa wahamaji, utoaji wa mafunzo ya kiuhamiaji, kwa mara ya kwanza, Idara ya Uhamiaji, imeanzisha chuo chake cha mafunzo, eneo la Kichakamiba, Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga.

Lengo la kuanzishwa kwa chuo hicho ni kutoa mafunzo mbalimbali kwa Maafisa na Askari wa Uhamiaji ili kuwawezesha kutoa huduma bora na zinazokidhi viwango vya Kitaifa na Kimataifa, na hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wetu katika mtazamo wa uhamaji wa watu.

Siku ya Kimataifa ya Wahamaji Duniani ilianza kuadhimishwa mnamo tarehe 04 Disemba 2000 kufuatia Azimio Na. 55/93 lililopitishwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa lengo la kutambua haki na mchango wa wahamaji pamoja na familia zao, Tangu kupitishwa kwa azimio hilo, nchi nyingi Duniani pamoja na Taasisi za Kimataifa, Taasisi za Serikali na Asasi zisizo za Serikali  zimekuwa zikiadhimisha siku hii muhimu kwa wahamaji, Kwa upande wa Idara ya Uhamiaji Tanzania, hii inakuwa ni mara yake ya tatu kuadhimisha siku hii Kitaifa. 

 HABARI PICHA NA MATUKIO

Mgeni Rasmi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene (katikati) akiwa katika Picha ya Pamoja na Makamishna Jenerali Wastaafu wa Uhamiaji (Waliosimama) sanjari na viongozi wa dini
Mgeni Rasmi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene (katikati) akiwa katika Picha ya Pamoja na Viongozi Waandamizi wa Uhamiaji (Waliosimama)Kushoto kwake ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala

Mgeni Rasmi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene (katikati) akiwa katika Picha ya Pamoja na Wawakilishi wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama 

Mgeni Rasmi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene akitoa Hotuba


CGI Dkt. Anna Makakala akitoa Maelezo mafupi ya Siku ya Kimataifa ya Wahamaji Duniani


Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wahamaji IOM Dkt. Qasim Sufi




Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania Mrakibu Paul Mselle


Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene akipata maelezo Elimu kwa umma kuhusu masuala ya Ki-uhamiaji kutoka kwa Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Azizi Kirondomara kutoka Kitengo cha Uhusiano


Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene akitoa pongezi kwa kikundi cha Uhamiaji Tanzania Live Band 




Uhamiaji Tanzania Band Ikitumbuiza





Msanii wa Bongo Fleva Beka akitumbuiza siku ya Kimataifa ya Wahamaji Duniani



















Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe.George Simbachawene akisalimiana na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala  


Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene akisalimiana na Dkt. Qasim Sufi


Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene akialimiana na Kamishna wa Uhamiaji Divisheni ya Vibali vya Ukaazi Pasi na Visa Mary Palmer (ndc)


Maandamano yakipita mbele ya Mgeni Rasmi




Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene akimkabidhi fedha Meneja wa Band ya Uhamiaji Mkaguzi Msaidizi Dennis Kimaro baada ya kufanya kazi nzuri 

 Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akimkabidhi Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene Vipeperushi vya huduma mbalimbali za Ki-Uhamiaji

Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene akifurahia jambo na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (Mstaafu) Victoria Lembeli, wa Kwanza Kulia ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiteta jambo na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Mstaafu Magnus P.J. Ulungi







Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akibadilishana mawazo na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wahamaji IOM Dkt. Qasim Sufi



Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiagana na awakilishi wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Nchini

Uhamiaji Tanzania Live Band wakiwa katika Picha ya Pamoja (Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni