Na Mwandishi Wetu, Mtwara Tanzania
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi James A. Mwanjotile amewaasa walimu wa Mkoa wa Mtwara kushirikiana na Idara ya Uhamiaji ndani ya mkoa huo katika kutoa taarifa za wahamiaji haramu wanaoingia nchini kinyume cha sheria.
Ameyasema hayo katika mkutano wa uongozi wa baraza la chama cha walimu Mkoa wa Mtwara baada ya kualikwa na kutumia fursa hiyo kutoa elimu juu ya ushiriki wa wananchi katika kulinda usalama wa nchi na mipaka yake.
Mkoa wa mtwara umepakana na nchi jirani ya msumbiji ambapo kumekuwa na matukio mbalimbali ya wahamiaji haramu kuingia nchini kupitia njia zisizo rasmi katika vijiji mbalimbali vinavyopakana na nchi jirani ya Msumbiji na baade kuleta madhara ya uhalifu ndani ya Mkoa wa Mtwara.
"Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwenu nyinyi wajumbe wa baraza la waalimu Mkoa, na wakaazi wa Mkoa huu ambao wengi wenu mnatoka maeneo ya mipakani tunaomba muweze kusaidia kutoa taarifa mbalimbali za wahamiaji haramu au pale mnapoona viashiria vyovyote vya watu msiowafahamu na mnashaka nao katika maeneo yenu tafadhali toeni taarifa mapema ili tuweze kuchukua hatua haraka iwezekanavyo, kwani jukumu la ulinzi wa nchi na Mipaka yake ni Jukumu letu sote”Alisema
Aidha amewasihi kuwa mabalozi wazuri kwa kuwaelimisha wanafunzi na wananchi wengine waishio maeneo mbalimbali ya Mkoa huo kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa zozote za wahamiaji haramu na hata pale watakapoona ama kuhisi mtu yeyote ambae si raia wa Tanzania ameingia nchini kinyume na sheria basi waweze kuwasiliana nae kupitia namba zake za simu ya mkononi alizozitoa au kuripoti katika ofisi yoyote ya Uhamiaji iliyopo karibu nae.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi James A. Mwanjotile akitoa Elimu ya Uhamiaji kwa Uongozi wa Baraza la Chama cha Walimu Mkoa wa Mtwara. |
Baadhi ya viongozi wa Baraza la Chama cha Walimu Mkoa wa Mtwara wakimsikiliza kwa makini Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi James A. Mwanjotile |
(Picha zote na Ofisi ya Uhusiano Uhamiaji Mkoa wa Mtwara) |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni