Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama
ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Victor Mwambalaswa imetembelea na kukagua
maendeleo ya Ujenzi wa jengo la Makao
Makuu ya Idara ya Uhamiaji jijini Dodoma leo Jumatatu Machi 16, 2020.
Kamati hiyo ambayo ilipokelewa na Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi Mhe. George Simbachawene , Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala,
Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Masoud Sururu, Kamishna wa Uhamiaji (Utawala
na Fedha) Edward Chogero pamoja na Maafisa Uhamiaji Waandamizi katika eneo la
ujenzi wa mradi huo.
Mhandisi Kanali Zabron Mahenge ambaye ni Meneja Mradi kutoka
Jeshi la Kujenga Taifa aliieleza Kamati hiyo kuwa ujenzi unaendelea vizuri pamoja
na kuwepo changamoto ndogo ndogo na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka
huu.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya Ujenzi huo, Mhandisi wa Mradi
David Pallangyo alisema hadi sasa ujenzi umefikia hatua nzuri ambapo sakafu ya
ghorofa ya tatu imekamilika kwa 60% na ujenzi utakamilika kwa muda uliopangwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Mhe.Mwambalaswa alimpongeza Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Kamishna Jenerali pamoja
na wahandisi kwa usimamizi mzuri ujenzi wa
Jengo hilo na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili ujenzi ukamilike
kama ilivyopangwa.
Nae Mjumbe wa Kamati hiyo ya Bunge Mhe. Almas Maige hakusita kutoa pongezi kwa Wizara ya mambo ya Ndani na Idara ya Uhamiaji
kwa ujenzi wa jengo hilo la Makao Makuu ambalo ni kubwa na la kisasa pindi
litakapokamilika.
Ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji jijini
Dodoma lenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 20 unaojengwa na Suma JKT unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa
mwaka huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni