Dar es salaam, Tanzania
Idara ya Uhamiaji Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni
ya mawasiliano ya Airtel mapema leo hii tarehe 5 Februari 2020 tumezindua
huduma ya malipo ya ada za pasipoti kwa njia ya Airtel Money ili kuongeza wigo wa malipo ya huduma za pasipoti.
Mgeni rasmi wa Uzinduzi huo Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Uhamiaji (SACI) Mohamed Awesu ambae pia ndie Mfawidhi Mkuu wa
TEHAMA Katika Jeshi la Uhamiaji Tanzania amesema Matumizi ya huduma hii
yatamrahisishia mwombaji wa pasipoti kufanya malipo kutoka mahali popote alipo.
“Ili kutumia huduma hii mteja anatakiwa kutembelea
tovuti ya Idara ya Uhamiaji (www.immigration.go.tz), atajaza fomu yake na
baada ya kukamilisha kujaza atapatiwa Namba ya Kumbukumbu ya malipo (Control
Number) ambayo ndiyo ataitumia kufanya malipo kwa njia hiyo ya Airtel Money. Baada ya hapo ataiprint
na kisha kuiwasilisha fomu hiyo katika Ofisi ya Uhamiaji kwa taratibu
zinazofuata” alisema.
Hatua ya kutumia huduma hii ya Airtel Money ni utekelezaji wa sera ya Serikali ya kwa taasisi zake
zote kufanya malipo ya huduma mbalimbali kupitia Mfumo wa Serikali wa malipo
kwa njia ya Mtandao GePG.
Mfumo huo umerahishisha sana malipo na umekuja na
faida nyingi kama vile kurahisisha malipo, kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu,
kupunguza upotevu wa mapato ya Serikali, kuondoa mianya ya rushwa pamoja na
kuongeza mapato ya serikali.
Aidha SACI Awesu ameipongeza Kampuni ya Airtel Tanzania kwa kuweza kuungana na
Huduma za Uhamiaji kama ilivyo kwa mitandao mingine ya mawasilano hapa nchini ili
kuwawezesha Watanzania kufanya malipo ya pasi za kusafiria kwa kutumia huduma
ya “Airtel Money”, hatua hii
inaendelea kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma ya Pasipoti.
Kwa Upande wake Mkurugenzi
wa Airtel Money Tanzania Bw. Isack Nchunda, amemshukuru Kamishna
Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala kwa ushirikiano mkubwa aliouonesha wakati wote wa
mchakato wa kuelekea tukio hili la ufunguzi wa huduma hii ili kuwarahisihia
wananchi kupata huduma ya pasipoti kwa urahisi na kufanya malipo sehemu yoyote
ile.
Bwana Nchunda aliongeza kuwa
mwombaji anaweza kulipa ada yake ya maombi ya
pasipoti baada ya kupewa kumbukumbu ya malipo (Control Number) ambapo
unapiga *150*60# Unachagua kufanya malipo Namba 5, Kisha unachagua malipo ya
serikali, halafu unaingiza namba ya kumbukukumbu ya malipo unaweka
kiasi kama ni ada ya fomu ya Pasipoti ambayo gharama yake ni Tsh 20,000tu na
ada ya Pasipoti baada ya kuprinti fomu zikishakaguliwa na Maafisa Uhamiaji
Unamalizia Tsh.130,000 tu ambayo huleta gharama ya pasipoti kwa Tsh. 150,000tu.
Sanjari na hilo unamalizia
kwa kuingiza namba zako za siri na kisha unathibitisha malipo yako na ndani ya
sekunde 10 mpaka 15 unapata ujumbe wa malipo yako kupokelewa.
Kampuni ya Mawasiliano ya
Airtel Money ni Kampuni inayomilikiwa na serikali kwa asilimia 49% ndio maana
inarahisisha maisha kwa kushirikiana na Uhamiaji, kuhakikisha watanzania
wanapata huduma bora kupitia Airtel Money kwa haraka na uhakika zaidi.
Mfumo wa Uhamiaji Mtandao ulizinduliwa rasmi na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli tarehe 31 Januari, 2018. Tangu wakati huo, fomu
za maombi ya Pasipoti zimekuwa zikijazwa kwa njia ya mtandao, Hivyo Uhamiaji
Tanzania inatoa wito kwa wananchi kuendelea kutumia huduma hii ya Airtel Money
katika kufanya malipo yao ya ada za pasipoti kwani ni salama na rahisi kutumia.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Huduma zikiendelea kutolewa kwa wateja kujua namna ya kulipia pasipoti kwa njia ya Airtel Money |
Mkurugenzi wa Airtel Money Tanzania Bw. Isack Nchunda akitoa maelezo mafupi ya namna ya kufanya malipo ya ada ya pasipoti kwa njia ya Airtel Money |
Afisa Uhusiano Mrakibu Msaidizi akiongoza itifaki katika tukio zima la Uzinduzi wa Huduma ya malipo ya ada ya Pasipoti kwa njia ya Airtel Money |
Uhamiaji Tanzania Jazz Band nayo haikubaki Nyuma ilisindikiza Tukio hilo kwa kutoa Burudani kabambe kwa wateja walihudhuria tukio hilo |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni